Shirika la Grumeti Fund kupitia Idara ya Maendeleo ya jamii, kituo cha Mazingira, limefadhili safari ya vijana wawili kutoka katika Shule za Sekondari Issenye na Natta za Wilayani Serengeti kwenda nchini Taiwan kwa ajili ya programu maalum ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora za utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
Msimamizi wa Kituo cha Mazingira Bw. Laurian Kahatano amebainisha kuwa, Flora Nyaboko Gesimba, Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Natta na Mkazi wa Kijiji cha Maburi pamoja na Cosmas Godfrey Kitena, Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Issenye na Mkazi wa Kijiji cha Singisi wamepata ufadhili wa safari hiyo baada ya kuibuka washindi katika shindano la uandishi wa
insha (Essay) lililohusisha wanafunzi 32 kutoka katika shule 16 zilizopo kwenye program ya Elimu ya Mazingira inayoendeshwa kwenye kituo chetu cha Mazingira (EEC).
"Hivi karibu tuliendesha mdahalo wa utunzi wa insha, katika shule zote 16 ambapo wanafunzi walipewa fursa sawa za kuweza kishiriki na katika ushirika huo, shule zililazimika kutoa washindi wawili wawili kwa upande wa kike na kiume na baada ya wanafunzi 32 kushindanishwa tuliweza kupata hawa washindi wawili ambao mbali na zawadi walizozipata pia wamepata safari ya kwenda nchini Taiwan ambapo walikaribishwa na shule moja iliyopo Taipei" alisema Bw. Kahatano
Aidha Bw. Kahatano ameongeza kuwa wanafunzi hao watapata fursa ya kutembelea vituo vya Utamaduni, vituo vya mazingira sambamba na kukutana na wabobezi katika masuala ya mazingira jambo litalowafungua fikra zao juu ya namna bora ya kuhusisha jamii na mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Grumeti fund Bi. Frida Mollel amewapongeza wanafunzi hao kwa kuibuka washindi katika shindano la uandishi wa insha na kupata ufadhili wa safari hiyo huku akiwataka kuitumia safari hiyo kama chachu ya mabadiliko chanya ya kifkira juu ya utunzaji wa mazingira na kuwataka kuwa mabolozi wazuri kampuni ya Grumeti fund.
"Ninawapongeza wanafunzi na wazazi kwa kupata nafasi hii adhimu kwani ni bahati na ni mpango wa Mungu kwenu ninyi wawili kupata nafasi hii, kupitia nafasi hii naomba mtumie safari hii kubadili fikra zenu juu ya utunzaji wa mazingira, kumbukeni mmebeba sura ya Grumeti huko muendako basi hakikisha mnakuwa mabalozi wazuri" alisema Bi. Frida
Kituo cha Elimu ya mazingira (EEC) chini ya Idara ya Maendeleo ya Jamii Grumeti Fund, kilianzishwa tarehe 8/12/2009 kikiwa na nia ya kufundisha vijana namna bora ya kuhifadhi rasilimali na utunzaji wa mazingira, ambapo kila mwaka kituo hicho kinafundisha vijana 512 kutoka katika shule 16 zilizopo pemboni mwa hifadhi ya taifa ya Serengeti kwa Wilayani za bunda na Serengeti.




Social Plugin