Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI HAI, FUONI , KATA TANO KUPIGA KURA KUCHAGUA WABUNGE NA MADIWANI KESHO



Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele leo Desemba 29,2025 amesoma risala maalum kuhusu uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Siha lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania Bara na Jimbo la Fuoni lililopo Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, Tanzania Zanzibar unaotaraji kufanyika Desemba 30,2025.

Jaji Mwambegele amesema, uchaguzi mdogo huo utahusisha pia, kata tano za Tanzania Bara. Kata hizo ni; Chamwino iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mkoa wa Morogoro; Mbagala Kuu iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam; na Nyakasungwa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa, Mkoa wa Mwanza.

Nyingine ni Kata ya Masoko iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mkoa wa Mbeya; na kata ya Ndono iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora.

Aidha, amesema jumla ya wagombea 33 kutoka katika vyama vya siasa 17 wanawania nafasi wazi za ubunge na udiwani katika maeneo niliyoyataja. Kati ya wagombea 33, wagombea 21 sawa na asilimia 63.64 ni wanaume na wagombea 12 sawa na asilimia 36.36 ni wanawake. Kwa namna ya pekee, Tume inavipongeza vyama vilivyoshiriki na wagombea waliojitokeza kushiriki.

Jaji Mwambegele amesema, jumla ya Wapiga Kura 218,024 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki katika uchaguzi huo na jumla ya vituo 556 vya Kupigia Kura vitatumika.

“Natumia fursa hii kuvikumbusha Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi kesho tarehe 30 Desemba, 2025 kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya zoezi la kupiga, kuhesabu na kujumlishia kura. Wasimamizi wa uchaguzi katika Majimbo na Kata husika, wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.

Amesema, mawakala hao, wanawajibika katika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu za Uchaguzi na maelekezo ya Tume katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni.















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com