
Mussa Azzan Zungu
**
Na Dotto Kwilasa - Malunde 1 blog Dodoma
Aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita na Mbunge wa Jimbo la Ilala kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Azzan Zungu, amechaguliwa kwa kishindo kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uchaguzi huo umefanyika jijini Dodoma, ambapo Zungu amepata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa na wabunge, huku kura tatu zikiharibika.
Matokeo hayo yamempa ushindi mkubwa uliomuwezesha kushika rasmi nafasi ya Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Zungu ameahidi kuongoza Bunge kwa uwazi, nidhamu na uwajibikaji, akisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha chombo hicho kinaendelea kuwa nguzo muhimu ya demokrasia na uwakilishi wa wananchi.
Kwa ushindi huo, Zungu anakabidhiwa jukumu zito la kusimamia mwenendo wa mijadala, kudumisha heshima ya Bunge, na kuhakikisha Serikali inawajibika ipasavyo kwa maslahi ya wananchi.
Katika uchaguzi huo, wagombea wengine walikuwa ni Veronica Tyeah (NRA), Anitha Mgaya (NLD), Chrisant Nyakitita (DP), Ndonge Ndonge (AAFP) na Amin Yango (ADC), ambapo wawili kati yao walipata kura moja moja, huku wengine wakikosa kura kabisa.
Social Plugin