Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga Joseph Swalala akizungumza na wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura katika ukumbi wa mikutano wa Masele ulioko Ukenyenge Tarafa ya Negezi wakati akifunga mafunzo hayo Oktoba 27,2025
Na Sumai Salum – Kishapu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewakumbusha wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni za Uchaguzi, ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unafanyika kwa uwazi, amani na uadilifu.
akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo ya siku mbili Oktoba 27,2025 Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kishapu Joseph Swalala ameeleza kuwa uteuzi wao umefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 76 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, huku INEC ikibainisha kuwa jukumu la kuratibu na kusimamia uendeshaji wa uchaguzi nchini limewekwa wazi katika ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Aidha Swalala, amewataka wasimamizi hao 1,726 watakaosimamia vituo 556 katika tarafa za Kishapu, Negezi na Mondo, kuepuka kuwa chanzo cha migogoro na badala yake washirikiane katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na haki.
“Msiwe chanzo cha migogoro, mkatende haki, kumbukeni kuhakiki vifaa kabla ya kuvipeleka vituoni na msome Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo yote iliyotolewa na Tume pia mna wajibu wa kisheria kutekeleza majukumu ya uchaguzi kwa niaba ya Tume katika vituo vyenu vya kupigia kura ndio maana mmeapa kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa pamoja na kiapo cha kutunza siri.” amesema Swalala.
Kwa upande wake, Afisa Uchaguzi wa Wilaya hiyo Mwl. Sigisbert M. Rwezaula amewataka wasimamizi wote kufika vituoni kwa wakati ifikapo tarehe 28 Oktoba 2025 saa mbili asubuhi, akisisitiza kuwa hakuna sababu yoyote itakayokubalika ya kuchelewa au kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Sambamba na hayo jumla ya kumbi sita zimetumika katika Jimbo la kishapu zikigusa tarafa zote za jimbo hilo, Tarafa ya Kishapu,Negezi pamoja na Mondo huku lengo la mafunzo hayo likiwa ni kuwakumbusha majukumu kuhusu uendeshaji wa Uchaguzi ngazi ya kituo.
Afisa Uchaguzi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Sigisbert M. Rwezaula akizungumza na wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura katika ukumbi wa mikutano wa Mwadui Lutheran ulioko Tarafa ya Mondo Oktoba 27,2025
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Atuganile Stephen akizunguza kwenye mafunzo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vya kuoigia kura wakati akitoa elimu ya makosa ya Rushwa kwenye uchaguzi
Social Plugin