Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDETTOSON AFUNGA KAMPENI KWA KISHINDO, AAHIDI KUENDELEA KUWATUMIKIA WANANCHI KWA NIDHAMU

Mgombea Udiwani wa Kata ya Kishapu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joel Ndettoson akizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya Kishapu Mkoani Shinyanga wakati akifunga kampeni zake Oktoba 26,2025 viwanja vya mabela

Na Mwandishi wetu

Mgombea Udiwani wa Kata ya Kishapu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joel Ndettoson, amefanya mkutano wa kufunga kampeni uliofurika wananchi katika uwanja wa Mashine za Mabela, Wilayani Kishapu, ambapo ametumia fursa hiyo kuelezea mafanikio aliyoyapata katika kipindi chake cha miaka mitano iliyopita na dhamira yake ya kuendeleza jitihada hizo kwa nguvu mpya.

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi na wanachama wa CCM, Oktoba 26,2025 Ndettoson amesema kipindi cha kwanza cha uongozi wake kimekuwa cha mafanikio makubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, miradi ya maji safi na salama, elimu na afya, sambamba na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya Serikali katika Kata hiyo.

“Nawashukuru wananchi wa Kata ya Kishapu kwa ushirikiano wenu mkubwa katika kipindi chote cha miaka mitano. Tumeweza kufanya mengi pamoja,lakini bado yapo machache tuliyoanza na ninadhamiria kuyakamilisha kwa nguvu mpya pindi mtakaponipa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia,” amesema Ndettoson.

Amesema kipindi hicho kimekuwa cha mafanikio makubwa kwa Kata ya Kishapu, ambapo miradi mingi ya maendeleo imekamilika chini ya ushirikiano wake na wananchi pamoja na Serikali ya CCM.

Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa kimeonesha dhamira ya dhati katika kuwaletea Watanzania maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi wa ngazi zote.

Kwa upande wao, wananchi waliohudhuria mkutano huo wamempongeza Ndettoson kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kuleta maendeleo, wakiahidi kumpa kura zote ili aendelee na kazi aliyoianza kwa uadilifu na uaminifu.






















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com