Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTATIRO : WANANCHI MSITISHWE NA TAARIFA ZA MAANDAMANO, HAKUNA MWENYE KUZUIA UCHAGUZI..."SHINYANGA IPO SHWARI"

Mkuu  wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewatoa hofu wananchi kuhusu uvunjifu wa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa wilaya hiyo ipo salama na maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya uchaguzi wa amani na utulivu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 27, 2025, Mtatiro amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wanashiriki zoezi la kupiga kura katika mazingira ya utulivu, huku akiwataka kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya kikatiba bila hofu.

“Nawaomba wananchi wa Shinyanga wasitishwe na taarifa zinazozagaa mitandaoni kwamba siku ya uchaguzi kutakuwa na maandamano. Hakuna maandamano yoyote yaliyopangwa. Tunayo amani, na amani hiyo ndiyo tutailinda siku zote,” amesema Mtatiro.

Ameongeza kuwa hakuna mtu wala kikundi chochote chenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi kufanyika, kwani ni takwa la kikatiba, na yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mtatiro pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha umoja, upendo na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea utulivu na mshikamano wa wananchi.

Aidha, amewahakikishia watu wenye ulemavu, wazee na wanawake wenye watoto wadogo kuwa watapewa kipaumbele wakati wa kupiga kura, kama sehemu ya kuhakikisha ushirikishwaji wa makundi yote katika mchakato wa kidemokrasia.

Ametaja idadi ya vituo vya kupigia kura wilayani humo kuwa ni 1,007, ikiwemo Shinyanga Mjini vituo 391, Solwa vituo 364 na Itwangi vituo 252.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ambapo Watanzania watawachagua Madiwani, Wabunge na Rais.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com