Baraza la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza limewaelekeza waumini wake nchini kuanza mfungo maalum wa maombi ya amani kuanzia Alhamisi, Oktoba 23, 2025 hadi siku yatakapotangazwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, amesema uamuzi huo umetokana na dhamira ya baraza hilo kuona Watanzania wote wanashiriki kuiombea nchi amani, umoja na mshikamano katika kipindi hiki cha uchaguzi.
“Tarehe 23 vituo vyetu vyote na misikiti yetu watafunga mpaka siku yatakapotangazwa matokeo. Ni maelekezo rasmi tumeyatoa,hakuna kitu kigumu kama kukubali njaa, lakini tutafunga kwa ajili ya nchi hii kwa sababu tunao wajibu wa kupigania amani yake,”amesema Sheikh Kabeke.
Amefafanua kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa historia ya viongozi wa dini kushiriki katika kudumisha amani na umoja wa kitaifa, akisema wazee wa imani mbalimbali walikuwa sehemu ya harakati za kuutafuta uhuru wa nchi, hivyo vizazi vya sasa vina jukumu la kuilinda.
Katika maelezo yake, Sheikh Kabeke amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa utulivu, na kugeuza Oktoba 29, 2025 kuwa siku ya vikao vya kifamilia vinavyokumbusha umuhimu wa kura, badala ya kushabikia miito ya maandamano au “ulinzi wa kura” unaosambazwa mitandaoni na baadhi ya wanasiasa.
Aidha, kiongozi huyo wa dini amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti, akisema amekuwa mfano wa hekima na uthabiti tangu alipolikabidhiwa taifa katika kipindi kigumu cha kiuchumi na kijamii.
“Dkt. Samia amebeba majukumu makubwa katika kipindi ambacho nchi ilikuwa imekumbwa na changamoto nyingi ameendeleza miradi iliyokuwa michanga na leo tunashuhudia utulivu, amani na maendeleo,”aliongeza Sheikh Kabeke.
Kwa mujibu wa BAKWATA Mwanza, mfungo huo wa maombi ni alama ya imani, mshikamano na uzalendo unaolenga kuendelea kuijenga Tanzania yenye amani na maelewano kati ya watu wa dini zote.



Social Plugin