Serikali imeanza utekelezaji wa mpango mkubwa wa kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mafuriko mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti athari za mvua kubwa na matukio ya hali ya hewa kama El-Nino na Kimbunga Hidaya.
Kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), miradi 13 ya dharura yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 119 inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili kurejesha mawasiliano na kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi bila vikwazo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa madaraja ya Kipwata, Mikereng’ende, Somanga Mtama na Njenga II kwenye Barabara Kuu ya Marendego – Lindi – Mingoyo, pamoja na miradi ya Boksi Kalavati katika maeneo ya Sakura, Songas na Mtandango.
Katika Barabara ya Mkoa ya Nangurukuru – Liwale, ujenzi unaendelea katika madaraja ya Miguruwe, Zinga na Kimambi, huku barabara ya Liwale – Nachingwea ikishuhudia kazi za ujenzi wa madaraja ya Nangano na Mbwemkuru II pamoja na makalavati ya dharura.
Aidha, TANROADS inaendelea na ujenzi wa madaraja ya Nakiu na Kigombo katika barabara ya Kiranjeranje – Namichiga, pamoja na makalavati sita katika barabara ya Tingi – Kipatimo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Msimamizi wa Kitengo cha Miradi ya Maendeleo TANROADS mkoa wa Lindi, Mhandisi Fred Sanga, alisema zaidi ya shilingi bilioni 58.5 zimeshalipwa kwa wakandarasi na utekelezaji unaendelea kwa kasi, ukitarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mhandisi Sanga, katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 16.2 kwa matengenezo na maendeleo ya barabara mkoani humo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kilomita 405.15 za lami na kilomita 901.54 za changarawe pamoja na madaraja matatu katika barabara za Kilwa Masoko – Liwale, Matangini – Chiola – Likunja na Chiola – Ruponda.
Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa za Oktoba 2023 hadi Mei 2024 yaliharibu kwa kiwango kikubwa miundombinu ya barabara mkoani Lindi, na kusababisha maeneo mengi kukosa mawasiliano.
Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilitenga shilingi bilioni 19 kwa ajili ya matengenezo ya dharura ili kurejesha miundombinu hiyo kwa haraka.



Social Plugin