Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUSHIRIKI UCHAGUZI KWA AMANI – DKT. SAADA MKUYA





Na Mwandishi wetu, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais  Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, amewataka Watanzania kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa vurugu na uvunjifu wa sheria havina tija kwa taifa bali huathiri ustawi wa jamii.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), tukio lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau wa sekta ya bima, Dkt. Mkuya alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu, kwani maendeleo hayawezi kupatikana bila amani.

“Uchaguzi bila vurugu inawezekana. Tushiriki kwa amani na tusivunje sheria, kwa sababu bima haiwezi kulinda madhara yatokanayo na fujo au makosa ya jinai,” alisema Dkt. Mkuya.

Aliongeza kuwa sekta ya bima imeendelea kukua kwa kasi nchini, ikichochea ustawi wa uchumi na kulinda mali za wananchi, lakini akakumbusha kuwa bima inalinda matukio halali pekee, si yale yanayotokana na uvunjifu wa sheria.

Hafla hiyo pia ilihusisha uwasilishwaji wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2024, ambapo Dkt. Mkuya alitumia fursa hiyo kuipongeza TIRA kwa jitihada za kusimamia ukuaji wa sekta hiyo na kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma za bima kwa ufanisi.

Waziri huyo alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi wote kushiriki uchaguzi kwa utulivu na kuendelea kulinda amani iliyopo, akisema ni msingi wa maendeleo endelevu na ustawi wa Taifa.










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com