Mgeni rasmi, Bi. Mariamu Mkali
*****
NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE
WAKAZI wa Chalinze mkoa wa Pwani wamehimizwa kujenga mahusiano mema baina yao na walimu ili kuinua kiwango cha taaluma shuleni.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Maftaha Plaza, Bi. Mariamu Mkali alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi katika mahafali ya kidato cha nne ya shule ya sekondari Chalinze jana.
Bi. Mariamu alieleza kwamba katika uzoefu wake mahali ambapo Kuna changamoto ya kutokuelewana mara kwa mara kati ya wazazi na walimu husababisha taaluma kuwa duni kwa wanafunzi.
Mkurugenzi huyo pia aliwahimiza wazazi na walimu kusimamia vema nidhamu ya wanafunzi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili ambao umekuwa tishio kubwa sana kwa vijana katika jamii katika siku za hivi karibuni.
Bi. Mariamu ambaye pia ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Bagamoyo aliwahamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ili kuchagua viongozi wanaoona wanaweza kuwaletea maendeleo kupitia sanduku la kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.
Naye mkuu wa shule hiyo Mwalimu Melkisedek Komba aliisifu Serikali, wadau wa elimu, taasisi mbalimbali na wananchi kwa kuchangia maendeleo ya elimu katika shule hiyo.
" Pamoja na changamoto mbalimbali shuleni hapa Lakini nipende kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mheshimiwa mbunge wetu(Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Chalinze na Waziri wa Kazi, ajira, vijana na wenye ulemavu) kwa kutupatia viti na meza 100 kwa matumizi ya wanafunzi wetu hivi karibuni", alisema Mwalimu Komba.
Aidha mkuu huyo wa shule alilishukuru shirika la CANFED kwa kuwapatia shilingi 14,400,000 huku wananchi na taasisi mbalimbali wakichangia michango mbalimbali iliyosaidia kuboresha miundo mbinu, kujenga na kukarabati samani za shule pamoja na maendeleo mbalimbali shuleni hapo.
Jumla ya shilingi 1,000,000 zilipatikana katika unadishaji wa keki. Kati fedha hizo taslimu shilingi 869, 000 na ahadi ni shilingi 131,000. Huku watahiniwa 289 walitunukiwa vyeti vya kuhudhuria na vile vya ubingwa katika idara mbalimbali ikiwa pamoja na taaluma, uongozi, nidhamu, afya na mazingira.











Social Plugin