Na Mwandishi wetu,
Viongozi wa jamii ya Kimasai wameahirisha rasmi zoezi la tohara kwa vijana takribani 2,000 lililokuwa lifanyike kuanzia Oktoba 21 hadi 30 mwaka huu, ili kutoa fursa kwa vijana hao kushiriki kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Tangazo hilo limetolewa leo, Oktoba 17, 2025, na Laigwanani Mkuu wa Jamii ya Kimasai nchini, Bwana Isack Ole Kisongo Meijo, wakati wa Baraza la Maigwanani Mkoa wa Arusha, lililohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla.
Ole Kisongo amesema uamuzi huo ni ishara ya uzalendo na utayari wa jamii ya Kimasai kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa kupitia uchaguzi wa amani.
“Hiyo siku ni takatifu kwa Taifa la Tanzania. Tumeambiana jamii ya Kimasai hatujawahi kushika mkia, tunataka kujitokeza kwa wingi kupiga kura. Ukifanya tohara sasa utapunguza kura, kwani mgonjwa atashindwa kwenda kupiga kura. Tunataka tushiriki sote kwa amani,” alisema Ole Kisongo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, aliwapongeza viongozi wa Kimasai kwa uamuzi wao wa hekima, akisema huo ni mfano bora wa uzalendo na uelewa wa kisiasa unaochochea amani na mshikamano katika kipindi cha uchaguzi.
“Nawashukuru kwa kutambua umuhimu wa amani na kazi nzuri ya maendeleo inayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Endeleeni kuwa mabalozi wa amani na hamasisheni wananchi wengine kujitokeza kupiga kura kwa utulivu,” alisema Makalla.
Aidha, RC Makalla aliwataka wananchi wa Arusha na maeneo jirani kuendelea kuwa watulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi, na mara baada ya kupiga kura kurejea majumbani mwao, huku akisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha hali ya amani inatawala mkoani humo.
Uamuzi wa kuahirisha tohara umepongezwa na wadau wa kijamii na kisiasa kama hatua chanya ya kuonyesha uelewa wa kijamii unaolenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani, huru na wa haki.




Social Plugin