Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDANI YA MIAKA MINNE YA DKT. SAMIA MADARAKANI, UCHUMI UMEPAA : PROF. ASSAD





Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, uchumi wa Tanzania umeonyesha ukuaji thabiti na unaovutia.

 Hii ni kauli ya Prof. Mussa Juma Assad, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) na Mkaguzi Mkuu Mstaafu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akizungumza kando ya kongamano la kitaaluma lililojadili Utekelezaji wa Uchumi Jumuishi kuelekea Dira 2050, Prof. Assad amesema kuwa uchumi wa nchi umekua kwa wastani wa asilimia 6, jambo linalorahisisha wananchi kupata mahitaji yao muhimu kama chakula, elimu na huduma nyingine za msingi.

 “Kwa jumla uchumi wa Tanzania umekuwa kwa wastani wa asilimia sita. GDP, kupanda na kushuka kwa pato la taifa kumekaa vizuri ukilinganisha na nchi jirani. Hali ya kiuchumi ni nzuri zaidi kuliko Kenya na Rwanda,” amesema Prof. Assad.

Profesa Assad ameeleza kuwa vigezo vya sasa vya kiuchumi vinaonyesha uwezo bora wa wananchi kuendesha maisha yao ukilinganisha na miaka ya nyuma, jambo linalothibitisha uimara wa uchumi wa taifa.

Hata hivyo, Prof. Assad amegusia changamoto ya vijana wahitimu vyuo vikuu kukosa ujuzi wa vitendo, akibainisha kuwa tatizo siyo kushindwa kupata ajira, bali ni ukosefu wa stadi za kazi.

 “Vijana wanapaswa kupewa mafunzo ya vitendo mara baada ya kumaliza masomo yao. Hii ni jukumu la serikali pamoja na sekta binafsi kutoa kozi fupi na fursa za mafunzo vitendo ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika sokoni,” amesema Prof. Assad.

Hii ni ishara ya wazi kwamba ukuaji wa uchumi lazima uende sambamba na ukuaji wa ujuzi na stadi za vijana, kwani bila vijana wenye ujuzi wa vitendo, taifa haliwezi kufanikisha malengo ya uchumi jumuishi na Dira 2050.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com