Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADIWANI SONGEA MJINI WAONESHA UMOJA,KAMPENI ZA CCM ZAZIDI KUSHIKA KASI MSHANGANO

Mgombea nafasi ya Udiwani kata ya Mshangano Benson Sovela akiwa anawasili eneo la uzinduzi wa kampeni katika kijiji cha Chandarua jimbo la Songea mjini 

Na Regina Ndumbaro Mshangano-Songea 

Katika harakati za uzinduzi wa kampeni za udiwani zinazoendelea katika kata mbalimbali za Jimbo la Songea Mjini, madiwani kutoka kata tofauti wameendelea kuonesha mshikamano mkubwa kwa kuungana kumuunga mkono mwenzao Benson Sovela, mgombea wa nafasi ya udiwani Kata ya Mshangano. 

Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 5, 2025 katika kijiji cha Chandarua na umehudhuriwa na wananchi wengi pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ni  Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, James Daniel Mgego, ambaye amemkabidhi rasmi Benson Sovela kitabu cha Ilani ya CCM kama ishara ya kuanza rasmi kampeni. 

Mgego ametumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba, akieleza kuwa amani na mshikamano ni nguzo kuu za maendeleo nchini. 

Aidha, ameonya dhidi ya propaganda za uchochezi zinazosambazwa mitandaoni na kuhimiza wazazi na wazee kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.

Katika hotuba yake, Benson Sovela amewaomba wananchi wa Kata ya Mshangano kumpa ridhaa ya kuwa diwani wao kupitia sanduku la kura.

 Ameahidi kuwa kiongozi wa watu wote bila kujali itikadi au tofauti zozote, huku akisisitiza kuwa maendeleo hayana chama na kwamba kazi nzuri ya CCM inapaswa kuungwa mkono. 

Ametaja mafanikio yaliyopatikana kupitia serikali ya CCM, hasa katika sekta za elimu na afya, kuwa ni ushahidi tosha wa dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo.

Benson Sovela pia ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Mshangano, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara hasa barabara ya Namanyigu–Mshangano, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yenye uhaba wa huduma hiyo. 

Amesema kuwa kupitia ilani ya CCM, miradi hiyo yote itatekelezwa kwa ufanisi iwapo atapewa nafasi ya kuwatumikia.

Uzinduzi huo umeonyesha si tu nguvu ya CCM katika Jimbo la Songea Mjini, bali pia mshikamano na umoja wa madiwani katika kuhakikisha kuwa kila kata inapata kiongozi makini na mwenye maono ya maendeleo. 

Wananchi wamehimizwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com