Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TIP YAONGEZA NGUVU KUPITIA VIJANA RIKA KISHAPU MRADI "CHAGUO LANGU, HAKI YANGU"

Mratibu Mwandamizi wa miradi Kutoka TIP Livinus Ndibalema akizungumza mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana rika kuhusiana na kutokomeza masuala ya ukatili wa Wanawake na Wasichana hasa wenye ulemavu kilichowakutanisha Viongozi wa Vijana wa Dini Septemba 4,2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga

Na Sumai Salum – Kishapu

Shirika la Tanzania Interfaith Partnership (TIP), ambalo linaundwa na Jumuiya za dini mbalimbali nchini na limekuwa mstari wa mbele katika kupinga mila na desturi kandamizi, limehitimisha mafunzo ya siku mbili kwa Viongozi wa madhehebu na Viongozi wa Vijana wa madhehebu ya Kikristo na Kiislam Wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga kupitia mradi wake wa “Chaguo Langu, Haki Yangu”.

TIP kwa miaka mingi limekuwa likishirikiana na viongozi wa dini, Serikali, wanaharakati na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa mpana juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, ukeketaji, pamoja na kuwajengea uwezo vijana na wanawake kushiriki ipasavyo kwenye maendeleo.

Akizungumza Septemba 4, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Kishapu, Mratibu Mwandamizi wa miradi TIP, Livinus Ndibalemwa, amesema kundi la vijana ni mhimili muhimu wa kuifikia jamii pana ambayo bado haijapata elimu ya kupinga ukatili, hasa wanawake na wasichana wenye ulemavu.

“Nataka mtambue kuwa kwa kuwa ninyi mnanafasi za uongozi katika nyumba za ibada na kwenye jamii zenu, ni wajibu wenu kuhakikisha mnaenda kusambaza elimu hii kwa nguvu zenu zote ili kuleta mabadiliko makubwa. Jamii yetu inapaswa kuondokana na ukatili na mila kandamizi zinazokandamiza haki za wanawake na watoto,” amesema Ndibalemwa.

Amesisitiza vijana hao kutumia majukwaa na mikutano ya kijamii na kidini kufikisha elimu waliyoipata, akibainisha kuwa nguvu ya vijana ikitumiwa ipasavyo inaweza kuibadilisha jamii kwa kasi.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Kishapu, Bernadetha Bagenzi, ambaye pia alikuwa Mwezeshaji, ameeleza umuhimu wa kushirikiana kwa vitendo ili kuleta matokeo ya pamoja.

“Elimu hii mliyoipata si ya kubaki vichwani mwenu pekee, bali itumike kwa utekelezaji wa pamoja. Hilo ndilo litakalotupa matokeo chanya katika kupiga vita mila na desturi kandamizi,” amesema Bagenzi.

Vijana walioshiriki mafunzo hayo wameipongeza TIP kwa kulitambua kundi hilo muhimu ambalo mara nyingi husahaulika katika mijadala ya kijamii, na wameahidi kutumia nafasi zao ipasavyo kuhakikisha jamii ya Kishapu inaondokana na ukatili, ndoa za utotoni na tamaduni kandamizi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamehitimishwa kwa azma moja kuu kuitumia sauti ya Vijana kama nyenzo ya kuibadilisha jamii na kuimarisha haki za Wanawake na wasichana Kishapu na Tanzania kwa ujumla.
Mwezeshaji wa mafunzo kutoka ofisi ya Maendeleo ya jamii Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Bernadetha Bagenzi akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo Vijana rika kuhusiana na kutokomeza masuala ya ukatili wa Wanawake na Wasichana hasa wenye ulemavu kilichowakutanisha Viongozi wa  Vijana wa Dini Septemba 4,2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani ShinyangaMratibu wa Mradi wa "Chaguo Langu Haki Yangu" (BAKWATA) unaotekelezwa na TIP kwa kushirikiana na UNFPA na HelpAge Salim A. Ibwe akifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo Vijana rika kuhusiana na kutokomeza masuala ya ukatili wa Wanawake na Wasichana hasa wenye ulemavu kilichowakutanisha Viongozi wa Vijana wa Dini Septemba 4,2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com