Na Kadama Malunde - Malunde
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imeendesha mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari mkoani humo, yakiwa na lengo la kuwajengea uelewa kuhusu makosa ya rushwa kwenye uchaguzi, sheria ya gharama za uchaguzi, na nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha uwajibikaji na uadilifu wakati wa uchaguzi.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Septemba 25, 2025 ,Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Bi. Mwamba Masanja, amewataka waandishi wa habari kutumia elimu hiyo kama nyenzo ya kuelimisha wananchi na kuchochea uwazi, uwajibikaji na uadilifu katika mchakato wa uchaguzi.
“Waandishi wa habari mna nafasi kubwa ya kusaidia kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa, lakini pia kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura ili taifa lipate viongozi bora na waadilifu,” amesema Bi. Mwamba.
Mafunzo hayo yalihusisha mada mbalimbali ikiwemo “Makosa ya Rushwa Kwenye Sheria ya Uchaguzi 2024” iliyowasilishwa na Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma, Mohamed Doo, na mada ya “Sheria ya Gharama za Uchaguzi” iliyowasilishwa na Mchunguzi wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Bi. Anicia John.
Akihitimisha mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa, Mohamed Doo amesisitiza kuwa vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya demokrasia, kwa kuwa vina nafasi ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira huru, ya haki na yasiyo na rushwa.
Kwa upande wake, Bi. Anicia John ameeleza kuwa tafsiri ya sheria ya gharama za uchaguzi inalenga kuimarisha demokrasia kwa kuweka mazingira sawa kwa wagombea, kudhibiti gharama za uchaguzi na kuondoa mianya ya vitendo vya rushwa.
Washiriki wa mafunzo hayo ya siku moja wameipongeza TAKUKURU kwa mpango huo na kuahidi kutumia elimu waliyopata kuelimisha jamii kuhusu madhara ya rushwa kwenye uchaguzi, ili kusaidia kujenga mazingira safi ya kidemokrasia.
TAKUKURU imekuwa ikiendesha mafunzo ya aina hiyo kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na kujenga jamii yenye maadili mema.


















































Social Plugin