
Malkia wa muziki wa Injili barani Afrika, Rose Muhando, ameendelea kuthibitisha nafasi yake katika tasnia ya muziki wa Injili baada ya kuachia video mpya iitwayo “Hatua” akiwa na mwimbaji mahiri kutoka Kenya, Victor Muthenya.
Wimbo huo mpya ambao umeanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, umetolewa rasmi kupitia mtandao wa YouTube na tayari umeanza kuvutia mashabiki wa muziki wa Injili kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika Hatua, Rose Muhando na Victor Muthenya wameunganishwa na sauti zenye nguvu na ujumbe wa kipekee unaohimiza hatua za imani, uthubutu na kutegemea nguvu ya Mungu katika maisha ya kila siku.
Video ya wimbo huo imepambwa kwa uimbaji wa hisia, mandhari yenye mvuto na ubora wa kisasa wa utayarishaji, hali ambayo imeongeza msisimko kwa mashabiki wa muziki wa Injili.
Rose Muhando, ambaye kwa muda mrefu amekuwa sauti ya matumaini na faraja kupitia nyimbo zake, ameendelea kuwavutia mashabiki kwa kutoa nyimbo zenye mafunzo na ujumbe mzito wa kiroho. Ushirikiano wake na Victor Muthenya katika wimbo huu unatarajiwa kuongeza ushawishi wa muziki wa Injili katika kanda ya Afrika Mashariki na zaidi.
Video ya Hatua inapatikana kupitia YouTube.
Social Plugin