Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MKUDE AFUNGUKA KUHUSU SIASA, UCHUMI NA MAENDELEO ARUSHA



Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mheshimiwa Joseph Modest Mkude, amefanya mkutano na waandishi wa habari leo Septemba 23, 2025, ambapo amezungumzia kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na siasa, uchumi, utamaduni na miradi ya maendeleo.

Katika taarifa yake, DC Mkude ameeleza kuwa hali ya kisiasa ndani ya Wilaya ya Arusha imeendelea kuwa tulivu na yenye ushirikiano kati ya vyama vya siasa, serikali na wananchi. Amepongeza pande zote kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa bila vurugu.

Kuhusu uchumi, Mkude amesema Wilaya ya Arusha imeendelea kustawi kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya utalii, kilimo na biashara ndogondogo. Amesisitiza kuwa mikakati ya kuongeza ajira na kipato kwa wananchi imepewa kipaumbele.

DC Mkude pia alizungumzia juhudi za serikali katika kukuza utamaduni wa Mtanzania kwa kuanzisha vikundi vya vijana vinavyohusiana na sanaa na michezo, kama njia ya kujenga mshikamano na ajira mbadala.

Katika suala la elimu, alisema serikali inaendelea kujenga shule mpya, kuongeza madarasa na kutoa vifaa vya kujifunzia ili kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa Arusha.

Akiangazia sekta ya afya, alisema serikali imetekeleza uboreshaji wa vituo vya afya, upatikanaji wa dawa muhimu pamoja na kuongeza watumishi wa afya katika maeneo ya vijijini.

Aidha, alieleza kuwa miradi mikubwa ya kimkakati inatekelezwa wilayani humo, ikiwemo ujenzi wa barabara, mabwawa ya maji na miundombinu ya umeme vijijini, kama sehemu ya mpango wa kuinua uchumi wa wananchi.

Mkude amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na vyombo vya habari, akisema waandishi wa habari ni daraja muhimu la kuwasilisha taarifa sahihi kwa umma na kusaidia maendeleo ya nchi.

Katika kipengele cha mazingira, amehimiza wananchi kuendelea kushiriki katika kampeni za usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, huku akiwasihi kuona taka kama rasilimali.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com