Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt.Mussa Ali Mussa Akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa shirika la viwango Tanzania (TBS)katika vibanda vya nanenane Morogoro
Na Mwandishi wetu Malunde 1 Blog-Morogoro
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa juhudi zake katika kuwahudumia wananchi, hususani wajasiriamali na wazalishaji wadogo, kwa kuwawezesha kupata alama ya ubora bila gharama yoyote.
“Kupitia TBS, bidhaa zetu zinaendelea kupata ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Hili ni jambo muhimu kwa uchumi wetu na kwa maendeleo ya wajasiriamali wetu,” amesema Dkt. Mussa.
Aidha, amelitaka shirika hilo kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya kilimo na viwanda katika kutoa elimu kwa wakulima na wazalishaji ili waweze kuongeza thamani ya bidhaa zao kwa kuzingatia viwango vya ubora.
Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TBS Kanda ya Mashariki, Sileja Lushibika, amesema shirika linaendelea kupanua huduma zake kwa kuhakikisha linawafikia wadau kupitia ukaguzi wa bidhaa viwandani na sokoni, utoaji wa mafunzo, pamoja na elimu kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Lushibika amesema TBS inawasaidia wajasiriamali kupata alama ya ubora bila malipo kwa kipindi cha miaka mitatu, ambapo wanapaswa kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
“Tunatumia Maonesho haya kama jukwaa muhimu la kutoa elimu kwa umma kuhusu uzalishaji wa bidhaa bora, kuonyesha teknolojia mpya, na kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda na biashara,” ameongeza Lushibika.
TBS ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazoshiriki Maonesho ya Nane nane mwaka huu, yakihusisha wakulima, wazalishaji na taasisi mbalimbali za maendeleo kutoka mikoa yote ya Kanda ya Mashariki.
Social Plugin