Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TARI YATOA ELIMU KWA WAKULIMA NANE NANE MBINGA YASISITIZA MATUMIZI YA MBEGU BORA KWA KILIMO CHENYE TIJA

Baadhi ya wakulima wakipata elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora zilizofanyiwa utafiti 

Na Regina Ndumbaro-Mbinga 

Katika maonyesho ya wakulima ya Nane Nane yanayoendelea Wilayani Mbinga, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia Kituo chake cha Naliendele Mkoani Mtwara, imejikita katika kutoa elimu kwa wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu matumizi ya mbegu bora zilizofanyiwa utafiti.

Lengo ni kuwawezesha wakulima kuongeza tija kwenye uzalishaji na kufikia mafanikio ya kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa.Mtafiti wa Kilimo wa TARI Stella Massawe amesema wakulima wengi bado wanategemea mbegu za kienyeji zisizokuwa na tija, hivyo TARI imeshiriki kwenye maonyesho hayo ili kuwajengea uelewa wa kutumia mbegu bora, hasa kwa mazao ya kimkakati kama korosho, karanga, ufuta na nyinginezo. 

Ameeleza kuwa hadi sasa TARI imezalisha aina 62 za mbegu bora za korosho ambazo zimeanza kutumika nchini, sambamba na kuwepo kwa vituo 17 vya utafiti na ushauri wa kilimo kote Tanzania, ikiwemo vituo vitano katika Mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake mtaalamu wa kilimo kutoka TARI Juma Mfaume amesema taasisi hiyo imewasilisha mbegu mbalimbali za nafaka kama vile mtama, ulezi na njugu mawe kwa kuwa zinahitajika sana na wakulima wa Nyanda za Juu Kusini. 

Ameongeza kuwa kupitia elimu hii, wakulima wataweza kubadilisha mitazamo yao kuhusu kilimo na kuanza kutumia teknolojia na mbegu zilizo bora zaidi kwa maendeleo yao na Taifa.

Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Mbinga, Onesifol Mlimba, amesisitiza kuwa maonyesho ya mwaka huu ni fursa adhimu kwa wakulima na wataalamu wa kilimo kupata mbinu bora za kilimo, hasa kwa mazao yanayostawi mkoani Ruvuma kama muhogo. 

Amebainisha kuwa elimu inayotolewa na TARI itasaidia viongozi na wakulima kuwa mabalozi wa kilimo bora katika maeneo yao, hivyo kuchochea mapinduzi ya kilimo na kupunguza umaskini vijijini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com