Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAELEZA MAFANIKIO SEKTA YA AFYA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya nchini kupitia uwekezaji wa vifaa tiba, miundombinu na rasilimali watu.

Akizungumza leo Agosti 15, 2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma, Msigwa amesema maboresho hayo yamewezesha upatikanaji wa dawa, vifaa na huduma muhimu kufikia ngazi ya vijiji na vitongoji.

“Serikali imeimarisha mfumo wa upatikanaji dawa kwa kuhakikisha MSD inasambaza bidhaa za afya kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa. Hatua hii imepunguza kwa kiwango kikubwa changamoto ya uhaba wa dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati,” alisema Msigwa.

Aliongeza kuwa pamoja na upatikanaji wa dawa, Serikali imeendelea kujenga na kukarabati vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa, sambamba na kuongeza idadi ya watumishi wa sekta hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila vikwazo.

Msigwa pia alisisitiza kuwa mafanikio haya yanatokana na usimamizi thabiti wa rasilimali na dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia huduma za afya zenye viwango vya juu.

Kwa mujibu wa Msigwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kujali eneo analoishi.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com