Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Katika jitihada za kuongeza ajira, kukuza viwanda vya ndani na kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi na zao la Korosho, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanza mkakati mpya wa kuongeza usindikaji wa korosho ndani ya nchi .
Akizungumza jijini Dodoma Agosti 22,2025 katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Korosho, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema Serikali imeanza kwa kusambaza mashine 200 za kubangua korosho katika mikoa inayolima zao hilo kwa wingi.
Amesema ashine hizo zitagawiwa kupitia halmashauri badala ya vikundi moja kwa moja, ili kuhakikisha matumizi endelevu na usimamizi wa karibu.
“Mahitaji ya mashine ni makubwa, na tumeamua kuanza na 200 kwa kuwa ni hatua ya kuelekea kutatua changamoto ya kuuza korosho ghafi nje ya nchi. Tunataka usindikaji uanze hapa hapa nchini,” amesema Waziri Bashe.
Bashe amefafanua kuwa mpango huo unalenga kusitisha kabisa uuzaji wa korosho ghafi nje ya nchi ili kuongeza thamani na mapato kwa wakulima, huku akisisitiza kwamba korosho kwa sasa inaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni kuliko mazao mengine, likiwemo tumbaku.
Katika kuhakikisha uzalishaji wa korosho unaendelea kwa tija, Waziri Bashe alizielekeza halmashauri zote kuanzisha vitalu vya miche ya korosho ambavyo vitawashirikisha wanawake na vijana, kama sehemu ya kuwawezesha kiuchumi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema mkoa wake umeanza rasmi kilimo cha korosho na unaamini utakuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa nchini.
“Tunakwenda kupindua meza, Singida tunalenga kuwa namba moja kitaifa kwenye uzalishaji wa korosho,” alisema Dendego kwa kujiamini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Francis Alfred, aliwahakikishia wadau kuwa bodi inaendelea kuimarisha masoko na kuweka mikakati ya muda mrefu kwa msimu wa 2025/2026.




Social Plugin