Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UWANJA WA NSEKELAA KUJENGA MSHIKAMANO WA MICHEZO KYERWA



Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajjat Fatuma Mwassa (wa kwanza mkono wa kulia) wakati wa Uzinduzi wa Uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu


Na Mariam Kagenda _Kagera  


Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa amezindua rasmi uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu ujulikanao kama Nsekela Stadium uliojengwa na Abdulmajid Nsekela Mwenyekiti wa taasisi ya Abdulmajid Nsekela Foundation. 

Akizindua uwanja huo uliojengwa Wilayani Kyerwa mkoani Kagera  katika eneo la Rwenkorongo  Mkuu wa Mkoa  Mwassa amempongeza Abdulmajid Nsekela mzaliwa wa  Kyerwa kutekeleza kwa vitendo  wito wake wa "Ijuka Omuka" kwa kukumbuka nyumbani na kuwekeza katika mradi mkubwa unaokwenda kuinufaisha jamii ya Wanakagera.


"Uwanja huu nauangalia kwa jicho la tatu wananchi wa Wilaya ya Kyerwa wamepata fursa ya kufanya mazoezi wakiwemo wanafunzi wa shule jirani hapa, pia taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi aidha kupitia mashindano mbalimbali tutaweza kupata burudani hapa badala ya kwenda mbali na Wilaya yetu." Alisema Mwassa.

Mkurugenzi wa Nsekela Foundation Abdulmajid Nsekela  alisema kuwa uwanja huo ameujenga kupitia Taasisi aliyoianzisha mwaka 2024  ya Abdulmajid Nsekela Foundation na ujenzi wa uwanja huo ni lengo mojawapo kati ya malengo nane yaliyomfanya kuianzisha taasisi hiyo.


Akiyataja malengo nane ya taasisi ya Abdulmajid Nsekela Foundation  Nsekela amesema ni Elimu, Ujasiliamali, kuwezesha vijana kiuchumi, Afya ya mama na mtoto, Uongozi, Utawala bora, Ustawi wa jamii pamoja na  Michezo na burudani huku akisema kuwa  amenza na michezo kwa kuwa inawaleta watu wengi kwa muda mfupi.


Ujenzi wa uwanja wa Nsekela Stadium ni uwanja wa mpira wa miguu ambao utajumuisha pia viwanja vya mpira wa mikono na kikapu ikiwa ni pamoja na eneo la  mashindano ya riadha na  kukamilika kwa uwanja huo utajumuisha ujenzi wa majukwaa ya watazamaji na uzio wa ukuta



Uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu wa Nsekela Stadium baada ya kuzinduliwa .

Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajjat Fatuma Mwassa akizindua Rasmi uwanja wa Nsekela Stadium.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com