
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekamilisha zoezi la kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa nafasi ya Ubunge katika Majimbo ya Kahama Mjini, Msalala na Ushetu mkoani Shinyanga, ambapo wanachama wake walijitokeza kwa wingi kuwachagua wawakilishi wao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga, amesema katika Jimbo la Kahama Mjini, jumla ya kura 6,195 zilipigwa, kura halali zikiwa 6,045 huku kura zilizoharibika zikiwa 80.
Benjamin Lukubha Ngaiwa ameibuka kinara kwa kupata kura 2,093, akiwashinda Sweetbert Charles Nkuba aliyepata kura 1,389, Jumanne Kibela Kishimba aliyepata kura 1,144, Francis Fikili Mihayo kura 821, Juliana Kajala Pallangyo kura 256, James Daudi Lembeli kura 219 na David Anyandwile Kilala aliyepata kura 191.
Kwa upande wa Jimbo la Msalala, jumla ya kura 7,845 zilipigwa, ambapo kura halali ni 7,685 na zilizoharibika ni 160. Mabula J. Magangila ameongoza kwa kura 5,518, akifuatiwa na Ambrose N. Nakale kura 929, Ezekiel Maige kura 791, Simon James Lufega kura 189, Edson Simba Masondole kura 152 na Ramadhani Shiganza kura 105.
Wakati huo huo, CCM Wilaya ya Kahama imemtangaza Emmanuel Peter Cherehani kuongoza katika matokeo ya awali ya kura za maoni Jimbo la Ushetu, huku matokeo ya mwisho yakisubiriwa kutokana na marudio ya uchaguzi katika kata tatu; Ubagwe, Mapamba na Bulungwa kufuatia malalamiko ya baadhi ya wanachama.

Hadi sasa, Emmanuel Cherehani ameongoza kwa kura 5,656, akiwashinda Valelia Wilson Mwampashe aliyepata kura 153, Machibya Mwambilija Dofu kura 171 na Mussa Shilanga Misungwi kura 452.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga, amewataka wanachama na wagombea wote kuwa watulivu na kusubiri maamuzi ya mwisho ya vikao vya chama kwa nidhamu na ustaarabu, kulingana na maadili ya CCM.


Social Plugin