Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC KIHONGOSI AANZA KAZI RASMI ARUSHA, AAHIDI KUPAMBANA NA VIKWAZO VYA MAENDELEO ARUSHA

 

 

Na Woinde Shizza , Arusha 

Kenan Laban Kihongosi, Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha Jumatatu Juni 30, 2025 ameanza kazi Rasmi Mkoani Arusha, akikabidhiwa Ofisi na Mtangulizi wake Mhe. Paul Makonda.

Katika siku yake ya kwanza, Kihongosi amezungumza na mamia ya wananchi waliokuja Kumlaki kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa lakini pia amezungumza na watumishi wa Mkoa wa Arusha. Lengo ni kupeana mwelekeo na kuwa na uelewa wa pamoja katika kuijenga Arusha na kuwaletea wananchi maendeleo.

"Tutakutana site, tutafanya ziara, tutakagua miradi, tutasikiliza kero, tutafanya ziara Wilaya zote, Halmashauri zote, Kata zote na tukimaliza tutakuja Mtaa kwa Mtaa. Hatutamuacha mtu nyuma. Huu ni mwaka wa uchaguzi, Viongozi bora wakatambulike kwa vitendo na sio maneno, tushiriki kwenye Uchaguzi Kikamilifu." Amesema Kihongosi.

 Kihongosi amesisitiza kuwa ametumwa Arusha kuja kuwatumikia wananchi katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo, akiomba Kila mwananchi wa Arusha kutoa ushirikiano katika kufikia maendeleo.

"Sitaruhusu kikwazo chochote kitakachojaribu kuzuia maendeleo ya wananchi, tunataka wananchi wawe na Imani na serikali yao." Amesema.

Amebainisha pia umuhimu wa Watumishi wa Umma, Viongozi wa kuchaguliwa na wale wa kuteuliwa kushirikiana na kushikamana, akiwataka kipaumbele kikuu kiwe kutekeleza kikamilifu matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan na kuitenda kazi ya kuwahudumia wananchi wa uaminifu.

"Huna sababu ya kugombana, kuumiza watu, kuwasema watu vibaya ama kutengenezea watu ajali. Sisi tunasema wajibu wetu ni kumuachia Mungu atimize yale aliyoyapanga"

 Kihongosi pia amesisitiza juu ya kila mmoja kuwa mlinzi wa amani na utulivu wa Mkoa wa Arusha, akieleza kwamba amani ndio msingi mkuu wa maendeleo na ustawi wa watu wa Arusha,hivyo amewahimiza kujiepusha na ushawishi wa baadhi ya watu wenye nia ovu na ambao watataka kutumia uchaguzi Mkuu ujao kuhamasisha vurugu na migawanyiko kwenye jamii.

"Hatutakubali michezo iliyokuwa inafanyika hapa, tunahitaji maendeleo, hatuhitaji kelele ama vurugu, tunahitaji amani, upendo na mshikamano."

Kihongosi pia amehimiza kuhusu upendo, kutofanya kazi kwa kushindana pamoja na kuoneana huruma, akihimiza kujiepusha na kuumiza watu ama kuharibia watu Maisha.

"Tufanye kazi kwa kuoneana huruma, kila mmoja ajue ana wajibu wa kumuonea mwenzie huruma, tusifurahi watu wakaharibikiwa mikononi mwetu, kila mmoja ana maisha, kila mmoja ana familia, kila mmoja ana watu wanaomtegemea. Wajibu wetu uwe kushirikiana na kupendana na kusaidiana. Tukawe walezi zaidi kuliko watu wa kushughulikiana." Amesisitiza Mhe. Kihongosi.

Mhe. Kihongosi awali aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha kwa kipindi cha mwaka Mmoja (2020) na wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Viongozi wengine walioteuliwa wakati Mhe. Kenani anahamishwa kutoka Simiyu kuja Mkoani Arusha, Rais Samia Suluhu Hassan alimsisitiza kuhusu kuja kuunganisha Jamii ya Arusha pamoja na kuhakilisha amani na utulivu unakuwepo wakati wote wa uchaguzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com