Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Katika kuhakikisha jamii inapata taarifa zilizo sahihi na zenye usawa kuhusu mwenendo wa haki nchini, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), imeendesha mafunzo ya kitaalamu kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuripoti habari za kimahakama kwa weledi.
Mafunzo hayo, yamefanyika kwa njia ya mtandao Julai 25, 2025, yamehusisha zaidi ya waandishi 170 kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Yameelezwa kuwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Mahakama kuhakikisha waandishi wanakuwa sehemu ya mfumo wa haki, kwa kutoa taarifa sahihi, zenye mizania na zisizopotosha.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, alisema waandishi wana mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa taswira ya Mahakama mbele ya umma.
“Habari moja yenye makosa ya alama au tafsiri potofu inaweza kuharibu heshima ya mhusika au kuzua taharuki isiyo ya lazima,” alisema Prof. Ole Gabriel.
Katika mafunzo hayo, Wakili wa Mahakama Kuu na mwandishi mkongwe, Bw. Alloyce Komba, alifafanua kwa kina umuhimu wa uelewa wa muundo wa Mahakama kwa waandishi.
Alitoa mfano wa kosa la kawaida ambapo baadhi huandika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, badala ya jina sahihi Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, na kueleza kuwa usahihi huu ni sehemu ya uadilifu wa kazi ya uandishi.
Aidha, aliwahimiza waandishi kutambua vyanzo halali vya taarifa za Mahakama, ambavyo ni pamoja na Majaji, Mahakimu, Makarani wa Mahakama, Waendesha Mashtaka, Mawakili na washtakiwa wenyewe.
Pia alikumbusha kuwa kazi ya mwandishi si kutoa hukumu au maoni, bali kuandika kile kilichotokea mahakamani kwa usahihi.
Kwa upande wake, Afisa Habari Mwandamizi wa Mahakama, Bw. Faustine Kapama, alisisitiza maadili ya uandishi wa habari za Mahakama, akitaja mambo yanayopaswa kuepukwa kama kuandika majina ya watoto, waathirika na mashahidi kwenye kesi za kingono au udhalilishaji.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yamefungua ukurasa mpya katika uhusiano kati ya Mahakama na wanahabari, huku waandishi wakipewa jukumu la kuwa daraja la haki – kwa kutumia kalamu zao kuelimisha, kuhabarisha na kulinda utu wa kila mmoja mbele ya sheria.

Social Plugin