Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ARUMERU WAITIKA KUCHUKUA FOMU KUWANIA UBUNGE



Na Woinde Shizza, Arumeru

Joto la kisiasa limepamba moto ndani ya Jimbo la Arumeru Magharibi, baada ya wagombea 21 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua fomu za kugombea ubunge huku baadhi yao wakigoma kuzungumza na waandishi wa habari kwa madai ya kufuata masharti ya chama.

Zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu limehitimishwa leo saa 10 jioni, ambapo idadi kubwa ya wanachama wamejitokeza kuwania nafasi hiyo, ikionesha hamasa kubwa miongoni mwa wanaCCM wilayani humo.
Baadhi ya wagombea walifika mapema kuchukua fomu huku wengine wakirejesha, lakini hali ya ukimya ilitawala kwa baadhi yao waliokataa kuzungumza na waandishi wa habari, wakisema kuwa wanazingatia maagizo waliyopewa na chama kuhusu utaratibu wa mchakato huo.

Miongoni mwa waliojitokeza ni John Tanaki Lazer, ambaye alisema ndoto yake ni kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi, akieleza kuwa ameanza safari hiyo kupitia familia yake na sasa anataka kuifikisha hadi ngazi ya ubunge.
“Kuibadilisha dunia huanzia chini, kwa mtu mmoja mmoja hadi familia. Siasa ni njia ya kuifanya dunia kuwa mahali salama kwa wote,” alisema Tanaki, akisisitiza umuhimu wa viongozi kutambua kuwa wao ni wasaidizi wa Rais katika kuleta maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru, Noel Emanuel Severe, ambaye naye amerejesha fomu leo, alisema kuwa alitekeleza zoezi hilo kimya kimya kama alivyoelekezwa na chama, bila kufanya shamrashamra zozote.

Severe aliongeza kuwa hana cha kusema kwa umma zaidi ya kumtanguliza Mungu na kukubali maamuzi ya vikao vya chama, akisema: “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”, akinukuu Wafilipi 4:13.

Kwa mujibu wa kamati ya uchaguzi ya CCM wilayani Arumeru, hatua inayofuata ni uchambuzi wa awali wa majina na uteuzi wa waliofanikiwa kuingia hatua ya kura za maoni, huku matarajio yakiwa makubwa kutoka kwa wanachama na wananchi wa jimbo hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com