Na Woinde Shizza, Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amezindua rasmi msimu wa tano wa kampeni ya Twende Zetu Kileleni, huku akiwataka Watanzania kuendeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutangaza utalii wa ndani na nje ya nchi kwa vitendo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo mkoani Kilimanjaro, Babu amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya asili vilivyopo nchini, akitolea mfano Mlima Kilimanjaro, akisema kuwa uko nyumbani na si wa wageni pekee.
“Ni muhimu sisi kama Watanzania tuwe wa kwanza kupanda mlima huu ambao ni kivutio kikubwa Afrika, tusiwaachie tu wageni, mlima huu ni wetu,” alisema Babu.
Aidha, aliwataka Watanzania kuwa na ari na morali ya kupanda mlima huo maarufu barani Afrika, huku akiwataka pia wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza mkoani Kilimanjaro, hasa katika sekta ya utalii na huduma.
Katika hatua nyingine, RC Babu alimtaka Mkurugenzi wa Zara Adventures kuendelea kuwekeza zaidi ndani ya mkoa huo, ikiwemo kujenga hoteli kubwa itakayoongeza thamani ya huduma za utalii kwa wageni na wazawa.
Alimpongeza pia kwa kuanzisha wazo la Twende Zetu Kileleni, kampeni inayolenga kupandisha Watanzania na wageni Mlima Kilimanjaro kila mwaka. Alisema kampeni hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza utalii na kuhifadhi mazingira.
Katika hotuba yake, Babu aliipongeza kampuni ya Utalii Zara Tours Adventures kwa mkakati wao wa kupanda miti katika maeneo ya hifadhi, jambo ambalo linasaidia kulinda mazingira na kuboresha hali ya hewa.
Akiwa anazungumzia mafanikio yaliyopatikana kupitia jitihada hizo, RC Babu alisema kampuni hiyo imepokea tuzo ya kimataifa kutokana na mchango wake katika kukuza utalii na kuhifadhi mazingira, akizipongeza pia TANAPA na KINAPA kwa uongozi bora uliosaidia ushindi huo.
Alieleza kuwa mafanikio ya sasa katika sekta ya utalii yametokana kwa kiasi kikubwa na video ya “The Royal Tour” iliyofanywa na Rais Samia, ambayo imevutia watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa kampuni ya Utalii Zara Tours Zainabu Ansell, alisema msimu wa tano wa Twende Zetu Kileleni umeboreshwa zaidi, ikiwemo kuwepo kwa huduma ya kwanza kupitia ‘clinics’ maalum kwa ajili ya wale wanaopanda mlima.
Alibainisha Msimu wa Tano wa twende zetu kileleni 2025 sasa unazidi kushika kasi kimataifa zaidi ya wageni 300 wanatatajiwa kupanda mlima Kilimanjaro huku watanzania wakiendelea kujivunia kampuni ya utalii ya ZARA .
“Tunazidi kuboresha tukio hili kila mwaka. Lengo ni kuwahamasisha Watanzania wengi zaidi kushiriki na pia kuvutia wageni, ili kuongeza pato la taifa kupitia fedha za kigeni,” alisema.
Naye Bernard Saini, Meneja wa Rasilimali Watu kutoka Zara, alibainisha kuwa msimu huu wa kupanda mlima unatarajiwa kuanza Desemba 5 hadi 10, mwaka huu. Alisema uzinduzi umefanyika mapema mwaka huu ili kupisha ratiba za kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Social Plugin