Mwanasiasa machachari na mmoja wa wanawake wachache waliopenya katika mchujo wa CCM, Susana Kululelela Nussu, ameidhinishwa rasmi na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kushiriki kura za maoni kwa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Ukerewe.
Susana, ambaye anaungwa mkono na wafuasi wengi jimboni humo, anatarajiwa kuingia katika kinyang’anyiro cha kisiasa dhidi ya wagombea sita wa kiume, hatua inayoashiria pambano kali la ndani ya chama. Wagombea wengine waliopitishwa ni: Dk. Switbert Zacharia Mkama, Joseph Michael Mkundi, Dk. Laurian Salvatory Mganga, Joshua Bituro Manumbu, Leonard Mujola Babilasi na Japhet Mtyama Kasiri.
Jimbo la Ukerewe limekuwa likibadilika mara kwa mara katika uwakilishi wake bungeni. Hata hivyo, mchakato wa mwaka huu unaleta sura mpya na ushindani mkali kati ya viongozi wapya na wale waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini na ndani ya chama.
Kwa Susana, nafasi hii ni mwanzo wa safari kubwa kisiasa. Endapo atashinda kura za maoni na kuungwa mkono na wajumbe wa CCM, atavunja historia kwa kuwa miongoni mwa wanawake wachache waliowahi kupeperusha bendera ya CCM katika kisiwa cha Ukerewe, eneo lenye historia ndefu ya siasa na mvuto wa kipekee.

Social Plugin