Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AZZA HILLAL HAMAD APETA JIMBO JIPYA LA ITWANGI, APITISHWA NA CCM KUWANIA UBUNGE



Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imempitisha Azza Hillal Hamad kugombea nafasi ya ubunge katika Jimbo Jipya la Itwangi, mkoani Shinyanga katika mchakato wa ndani ya chama.

Katika hatua hiyo ya awali ya mchakato wa ndani, Azza Hillal atachuana na wagombea wengine saba waliochujwa na kupitishwa na CCM. Wengine waliopitishwa ni Chrispine Myeke Simon, Sebastian Pastory Malunde, Fred Romanus Sanga, John Elias Ntalimbo, Christian Misobi Budoya, Hellena Daudi Mbuli, na Anna James Ng’wagi.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Julai 29, 2025, Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, alitangaza rasmi majina ya wanachama waliopitishwa kuwania nafasi za Ubunge wa Majimbo, Viti Maalum na Baraza la Wawakilishi, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Makalla amesema mchakato huo ulikuwa wa ushindani mkubwa na ulifanyika kwa umakini wa hali ya juu, baada ya kupokea zaidi ya maombi elfu tano kutoka kwa wanachama mbalimbali wa CCM, huku majimbo 272 ya Tanzania Bara yakihusika.


“Kwa wale ambao hawajapata uteuzi, niwaombe waendelee kuwa watiifu kwa chama, kwani bado CCM inawathamini na kuwatambua mchango wao,” amesema Makalla.

Makalla pia ameongeza kuwa uteuzi huo umezingatia vigezo vya uadilifu, kuchukuliwa na jamii, uwezo wa kiuongozi, pamoja na uwezo wa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM, huku akisisitiza kuwa chama kinajipanga kwa ushindani wa kweli kwenye Uchaguzi Mkuu.

Wagombea waliopitishwa katika hatua hii ya awali sasa wanatarajiwa kupigiwa kura na wajumbe wa CCM katika majimbo yao, ambapo mshindi mmoja kutoka kila jimbo atapitishwa  kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com