Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

FAHAD MUKADAM JINA HALIJARUDI...AMPONGEZA KAKA YAKE 'ABUBAKAR MUKADAM' KUTOBOA MBIO ZA UBUNGE SHINYANGA MJINI, AMTAJA KATAMBI, MASELE

 

Fahad Gulamhafiz Mukadam (kushoto) na Abubakar Gulamhafiz Mukadam (kulia)
****
Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa imepitisha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar Gulamhafiz Mukadam, kugombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini katika mchakato wa ndani ya chama.

Wagombea wengine waliopitishwa ni Stephen Julius Masele, Patrobas Katambi, Eustard Athanace Ngatale, Hassan Athuman Fatiu, Hosea Muza Karume na Paul Joseph Blandy.

Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa majina hayo, Fahad Gulamhafiz Mukadam, mdogo wa Abubakar Mukadam na ambaye pia alichukua fomu kugombea ubunge jimboni humo, ameandika taarifa kwa umma akielezea kukubali kwa moyo mkunjufu uamuzi wa chama wa kutomuingiza kwenye mchakato wa uchaguzi wa ndani.

Katika taarifa yake, Fahad amewashukuru wanachama wa CCM, viongozi na wananchi wa Shinyanga Mjini kwa imani na upendo waliouonyesha, na kupongeza kaka yake Abubakar Mukadam pamoja na wagombea wengine waliopitishwa, akisisitiza kuendelea kuwa mwaminifu kwa chama na kujiandaa kwa nafasi nyingine za kuwatumikia Watanzania.

“Kwangu, hii haikuwa mwisho wa safari, bali ni sehemu ya mchakato wa kujifunza, kujitathmini na kujiandaa kwa nafasi nyingine za kulitumikia Taifa. Kwa upendo, mshikamano, na mshikamano wa kweli  Tunasonga Mbele,” amesema Fahad.

Ujumbe wake unasomeka:

TAARIFA BAADA YA KUTOPITISHWA KWA MCHUJO WA NDANI WA CCM JIMBO LA SHINYANGA MJINI

Kwa heshima kubwa, napenda kuwashukuru wanachama wa CCM, viongozi na wapenda maendeleo wote wa Shinyanga Mjini kwa imani na upendo mliouonesha katika safari hii ya kutafuta ridhaa ya chama kupeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

Ingawa jina langu halikupendekezwa na Kamati Kuu ya CCM kuingia kwenye hatua ya upigaji kura wa ndani, naupokea uamuzi huo kwa unyenyekevu mkubwa, nikiwa na moyo wa kutii na kuendelea kuwa mtiifu kwa maamuzi ya chama changu.

Kwa moyo wa dhati, nampongeza kaka yangu Abubakar Gulamhafiz Mukadam pamoja na wagombea wengine waliopitishwa – akiwemo ndugu yangu Stephen Masele na Patrobas Katambi – kwa hatua hiyo muhimu. Ni imani yangu kuwa miongoni mwao atapatikana mshindi atakayeendeleza kazi kubwa ya ujenzi wa taifa letu, chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mimi binafsi nitaendelea kuwa mstari wa mbele katika kulitumikia Taifa letu na kuendeleza dhamira yangu ya kuwaletea Watanzania maendeleo kupitia nyanja mbalimbali, huku nikiwa mwaminifu kwa chama changu – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwangu, hii haikuwa mwisho wa safari, bali ni sehemu ya mchakato wa kujifunza, kujitathmini na kujiandaa kwa nafasi nyingine za kulitumikia Taifa.

Kwa upendo, mshikamano, na mshikamano wa kweli – Tunasonga Mbele.

Kwa Utii,

Fahad Gulamhafiz Mukadam
Shinyanga Mjini
29 Julai 2025

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com