Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anord Makombe
Msimamizi wa Uchaguzi, Katibu wa Vijana CCM Mkoa wa Shinyanga,Salama A. Mhampi akitangaza matokeo
Na Mwamvita Issa - Shinyanga
Viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Shinyanga Mjini pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa UWT, wametakiwa kuacha makundi ya kiushindani yaliyojitokeza wakati wa kura za maoni na badala yake kushikamana kwa lengo la kuimarisha nguvu ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Wito huo umetolewa Julai 21, 2025 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anord Makombe, wakati akihutubia mkutano huo maalum wa uchaguzi wa wagombea wa viti maalum vya udiwani, ambapo aliwataka viongozi na wanachama wote kuweka maslahi ya chama mbele.
“Ni muhimu kwa sasa kuacha tofauti, kujenga mshikamano na kuungana kama chama kimoja. Hii ndiyo njia ya pekee ya kuhakikisha tunashinda kwa kishindo nafasi za udiwani na ubunge,” amesema Makombe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini, Rehema Nhamanila, amewahimiza wanawake waliopitishwa kutumia nafasi hiyo vyema kwa kushirikiana na wanawake wengine kutafuta ushindi wa chama.
“Naomba tusahau yaliyopita, tuvunje makundi na sasa tuungane kwa pamoja. Ushindi wetu ni wa wote,” amesema Nhamanila.
Naye Msimamizi wa Uchaguzi, ambaye pia ni Katibu wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, Salama A. Mhapi, amesema uchaguzi huo maalum umezingatia misingi ya haki na usawa kwa wagombea wote, huku akiwataka waliokosa nafasi kutokata tamaa.
“Huu ni mwanzo tu. Tunatarajia kuwaona mkiendelea kushiriki nafasi nyingine ndani ya chama mwaka 2027,” amesisitiza Mhapi.
Kwa niaba ya madiwani waliopitishwa, Moshi H. Kazi kutoka Tarafa ya Mjini, aliwashukuru wajumbe kwa kuonyesha imani kwao, na kuahidi kufanya kazi kwa kushirikiana kwa maslahi ya wanawake na CCM.
“Tutahakikisha tunaliwakilisha vema kundi la wanawake ndani ya halmashauri kwa uadilifu,” amesema.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini kimeendesha uchaguzi wa ndani wa madiwani wa viti maalum kwa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, katika Tarafa mbalimbali, ambapo wanachama walijitokeza kwa wingi kushiriki mchakato huo muhimu uliofanyika Julai 20, 2025.
🔸 TARAFA YA MJINI
✅ Jumla ya wagombea: 18
✅ Kura zilizopigwa: 763
✅ Kura halali: 751
✅ Kura zilizoharibika: 12
✅ Idadi ya viti vinavyogombewa: 5
Washindi waliopatikana ni:
🔹 Moshi Husein Kanji – Kura 536
🔹 Ester Festo Makune – Kura 445
🔹 Veronica E. Masawe – Kura 431
🔹 Mwanakhamis Kazoba – Kura 355
🔹 Eunice Z. Manumbu – Kura 272
🔸 TARAFA YA OLD SHINYANGA
✅ Jumla ya wagombea: 3
✅ Kura zilizopigwa: 554
✅ Kura halali: 553
✅ Kura zilizoharibika: 1
✅ Idadi ya mshindi: 1
Mshindi aliyepatikana:
🔹 Mwanaidi Abdul Sued – Kura 539
🔸 TARAFA YA IBADAKULI (ZUHURA)
✅ Jumla ya wagombea: 3
✅ Kura zilizopigwa: 759
✅ Kura halali: 758
✅ Kura zilizoharibika: 1
✅ Idadi ya mshindi: 1
Mshindi aliyepatikana:
🔹 Zuhura Waziri Mwambashi – Kura 695
Mchakato mzima wa uchaguzi ulifanyika kwa amani na uwazi, ambapo wanachama walionyesha mshikamano na utayari wa kuendelea kujenga chama chao kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Ushindi wa wagombea hawa ni ushahidi wa imani kubwa waliyonayo wanachama kwao, huku wakiahidi kuendeleza sera na mwelekeo wa CCM katika kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com
Social Plugin