Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupinga Dawa za Kulevya Duniani, yatakayofanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Juni 24 hadi 26, 2025, jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amezungumza hayo leo June 24,2025 Jijini hapa na kuwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho hayo, akisisitiza kuwa janga la dawa za kulevya ni tishio kwa ustawi wa taifa, hasa kwa vijana ambao ndiyo tegemeo la nguvu kazi ya nchi.
“Ni muda wa Watanzania kuungana kwa pamoja kupinga janga hili,tunapaswa kulinda kizazi chetu kwa kuelimika na kuchukua hatua stahiki dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya,” amesema Mhe. Senyamule wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Maadhimisho hayo yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Jakaya Kikwete (JNICC), yataambatana na maonesho kutoka kwa taasisi mbalimbali zinazojihusisha na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, pamoja na kongamano maalum la vijana litakalojadili changamoto, fursa, na mbinu za kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii salama.
“Kupitia kongamano hilo, vijana wetu watajadili kwa kina nafasi yao katika mapambano haya, jambo litakalowasaidia kuwa sehemu ya suluhisho badala ya waathirika,” ameongeza RC Senyamule.
Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio katika vita dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufikiwa bila mshikamano wa kweli kutoka kwa jamii nzima. Alizitaka taasisi za umma na binafsi, viongozi wa dini, familia, na wanajamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kukomesha tatizo hilo.
“Hakuna taasisi au mtu mmoja anayeweza kushinda vita hii peke yake. Tunahitaji mshikamano wa kitaifa. Kila mmoja awe sehemu ya suluhisho kutoa taarifa, kuelimisha wengine, na kuwasaidia waathirika warejee katika maisha ya kawaida,” amesisitiza
Kwa mujibu wa RC Senyamule, maadhimisho ya mwaka huu ni ya kipekee kwa sababu yanaweka mkazo katika kuwajengea wananchi uelewa mpana wa athari za dawa za kulevya na kuhamasisha hatua madhubuti kwa ngazi zote za jamii.
Social Plugin