Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JICHO LA TAKUKURU KUELEKEZWA KWENYE MIRADI YA MAENDELEO NA WAGOMBEA UCHAGUZI 2025




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), ameielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha inasimamia kwa karibu na kwa uthabiti miradi yote ya maendeleo, akisisitiza kuwa miradi yenye viashiria vya rushwa haipaswi kuendelea, kwani inarudisha nyuma juhudi za Serikali na matarajio ya wananchi.

Akizungumza Juni 19, 2025, mara baada ya kutembelea banda la TAKUKURU katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Mhe. Kihenzile aliipongeza taasisi hiyo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa, hususan katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

“TAKUKURU hakikisheni mnatoa elimu muhimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kutoa na kupokea rushwa. Muwaelimisheni wasikubali kuchagua viongozi wanaonunua nafasi kwa kutoa rushwa, kwa sababu viongozi wa aina hiyo hawawezi kuleta maendeleo ya kweli,” alisema Mhe. Kihenzile.


Amesisitiza kuwa rushwa katika utekelezaji wa miradi ya Serikali ni sumu kwa maendeleo ya Taifa, hivyo ni wajibu wa TAKUKURU kuhakikisha kuwa fedha za umma zinalindwa ipasavyo, na kuwa miradi yote ya maendeleo inatekelezwa kwa uadilifu, uwazi na kwa viwango vinavyokubalika.

 “Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi. TAKUKURU hakikisheni mnasimama vyema kwenye nafasi yenu ili Taifa lipate viongozi waadilifu, na miradi ya maendeleo isibaki kuwa chanzo cha watu kujinufaisha binafsi,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uelimishaji Umma – TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Faustine Malecha, amesema taasisi hiyo inatumia maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kama jukwaa muhimu la kuelimisha jamii juu ya athari za rushwa katika uchaguzi na utekelezaji wa miradi ya umma.

 “Tunahakikisha wananchi wanajengewa uelewa juu ya haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi bora bila kushawishiwa kwa rushwa. Chaguo la viongozi kwa misingi ya hongo hudhoofisha maendeleo ya jamii nzima,” alisema Malecha.

Ameeleza kuwa TAKUKURU imejipanga kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa ukaribu zaidi, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo haigeuki kuwa mwanya wa kujipatia utajiri wa haramu, bali inakuwa na manufaa kwa wananchi wote.

 “Tutashirikiana kwa karibu na wananchi kuhakikisha kuwa kila hatua ya utekelezaji wa miradi inazingatia sheria, kanuni na maslahi ya Taifa,” amesisitiza.

Pamoja na shughuli nyingine, Wiki ya Utumishi wa Umma imeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za Serikali kutoa huduma, kuelimisha wananchi na kuonesha uwajibikaji katika utendaji wa kila siku.

Ushiriki wa TAKUKURU katika maonesho hayo umeongeza msukumo katika mapambano dhidi ya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com