Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MOI YAVUNJA MIPAKA YA TIBA, YAFIKISHA HUDUMA ZA KIBINGWA HADI MLANGONI




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Katika kile kinachoweza kutajwa kuwa ni hatua ya mfano na ya kuigwa katika sekta ya afya nchini, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeonesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia Watanzania wote bila kujali umbali wa makazi yao, kwa kuendelea kutoa huduma za kibingwa kupitia kliniki tembezi hata baada ya maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Kwa mara nyingine, MOI imeonyesha kuwa ubunifu katika utoaji wa huduma za afya unaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa maisha ya wananchi, hasa wale walioko nje ya jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Dodoma kwenye Wiki ya Utumishi wa Umma Dkt. Tumaini Minja, daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya mifupa, amesema kuwa kliniki hiyo tembezi inayohusisha madaktari bingwa imefanikiwa kuwahudumia wagonjwa zaidi ya 70 wa rika mbalimbali kutoka mikoa ya Kanda ya Kati.

"Tulikutana na wagonjwa wengi waliokuwa na maumivu ya mgongo, magoti na nyonga.

Lakini pia tumewahudumia wagonjwa waliowahi kutibiwa MOI na sasa wanaendelea vizuri. Hii imetuthibitishia kuwa matokeo ya tiba zetu yanaendelea kuwa chanya," amesema Dkt. Minja kwa msisitizo.

Kwa mujibu wa Dkt. Minja huduma hizo zinalenga kuongeza usawa katika upatikanaji wa huduma bora za afya nchini, ambapo kupitia kliniki tembezi, wataalamu wa MOI wanawafikia wananchi moja kwa moja katika mazingira yao, wakitoa ushauri, uchunguzi wa awali na tiba kwa magonjwa ya mifupa, mishipa ya fahamu na mgongo.

"Tunashukuru Serikali kwa kutuwezesha kuja mikoani. Dhamira yetu ni moja—kufikisha huduma hadi kwa mwananchi,hatuwezi kungoja wagonjwa wafike Dar es Salaam, bali sisi tunawafuata Kupitia Kliniki tembezi, "amesema

Huduma hiyo imepokelewa kwa furaha kubwa na wananchi wa Dodoma na mikoa jirani waliopata fursa ya kuhudumiwa moja kwa moja na madaktari bingwa, jambo ambalo limepunguza gharama na muda wa kusafiri kwenda MOI jijini Dar es Salaam.

Katika maonesho haya, MOI haikutoa tu huduma za afya, bali pia ilitoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na matatizo ya mifupa, umuhimu wa uchunguzi wa awali na mbinu sahihi za lishe na mtindo bora wa maisha.

Kwa ujumla, MOI imeonesha kuwa huduma za afya za kiwango cha juu zinaweza kutolewa hata nje ya hospitali kuu, na hivyo kuchagiza mageuzi ya sekta ya afya kuelekea katika mfumo wa huduma jumuishi na shirikishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com