Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIHENZILE: SEKTA YA UCHUKUZI IWE KITOVU CHA HUDUMA KWA WANANCHI



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), ametoa wito kwa watumishi wa umma kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kupitia sekta ya uchukuzi zinabeba tija, uadilifu na mwelekeo wa maendeleo kwa wananchi wote.

Ametoa kauli hiyo Juni 19, 2025, wakati wa ziara yake kwenye banda la Wizara ya Uchukuzi katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

 “Sekta ya uchukuzi inagusa maisha ya kila Mtanzania. Iwe ni barabara, reli, anga au majini — tunahitaji kuendelea kuboresha mifumo inayoweka mbele maslahi ya mwananchi kwa kuhakikisha huduma ni salama, za haraka na zenye tija,” alisema Kihenzile.


Amesema kuwa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni jukwaa muhimu la kutathmini uwajibikaji wa watumishi wa umma, na kwamba sekta ya uchukuzi ina mchango mkubwa katika kuharakisha ukuaji wa uchumi, hasa kwa kuchochea biashara na uwekezaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya karibu kati ya Serikali na wananchi kupitia maonesho hayo, akisema kuwa hatua hiyo hutoa nafasi kwa wananchi kuelewa vizuri huduma zinazotolewa na Serikali yao.

 “Katika wiki hii, ni muhimu kila mtumishi wa umma kujiuliza kama anamtumikia mwananchi kwa uadilifu, ufanisi na moyo wa kujitoa. Maadili, ubunifu na uwajibikaji ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli,” aliongeza.

Ziara ya Naibu Waziri Kihenzile katika banda la Wizara ya Uchukuzi imepokelewa kwa hamasa kubwa na wadau waliotembelea, ambapo watendaji wa wizara hiyo wameahidi kuendelea kutoa huduma bora zinazoendana na dira ya Taifa ya uchumi wa viwanda na usafiri endelevu.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com