Na Alex Sonna Dodoma
Tume ya Ushindani (FCC) imebainisha dhamira ya kuijengea jamii kizazi cha wataalamu wa ndani wa kutambua bidhaa bandia kwa kupendekeza kuanzishwa kwa kozi maalum ya uchunguzi wa bidhaa bandia katika vyuo vya elimu ya juu nchini.
Akizungumza jijini Dodoma kuelekea Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alisema elimu kwa vijana ni msingi wa muda mrefu katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia nchini.
“Tumeendelea kushirikiana na vyuo vikuu kama SUA, UDOM, UDSM, Mzumbe, St. Augustine na MUST katika utoaji wa semina juu ya athari za bidhaa bandia. Tunashauri elimu hiyo sasa ipewe nafasi katika mitaala ya kudumu,” amesema.
Ameeleza kuwa lengo ni kuandaa vijana wenye uelewa kuhusu miliki bunifu, haki za walaji, pamoja na athari za bidhaa bandia kwa afya na uchumi wa taifa, akisema: “Tunataka waelimike kabla hawajawa waathirika.”
FCC imeshatoa elimu kwa makundi mbalimbali yakiwemo viongozi wa serikali, wabunge, wafanyabiashara, wanahabari na mashirika ya kiraia.
Ngasongwa amesema hatua hiyo imeongeza ushirikiano wa kimkakati na taasisi za kikanda kama ZFCC ya Zanzibar na ACA ya Kenya.
Katika muktadha huo, FCC imetoa rai kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na vyuo husika kuanzisha kozi ya “Uchunguzi wa Ubora na Uhalisia wa Bidhaa” kwa ngazi ya stashahada na shahada.
Aidha, amesema wito huo unaendana na ajenda ya taifa ya kukuza uchumi wa ubunifu na maandalizi ya ushiriki madhubuti wa Tanzania katika Soko Huru la Afrika (AfCFTA) linalohitaji bidhaa bora na zenye viwango halali.
Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Juni 25, 2025 katika Ukumbi wa Mabeo, Dodoma, ambapo vijana kutoka vyuo mbalimbali wataonesha ubunifu wao kupitia mijadala na maonyesho ya bidhaa halali.
Social Plugin