
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewataka wateja wake wanaodaiwa kulipa madeni yao kwa hiari ili kusaidia Shirika hilo kujiendesha kwa ufanisi na kutoa huduma bora ya umeme kwa Watanzania.
Kupitia kampeni mpya iitwayo “Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie”, TANESCO inalenga kuhamasisha ulipaji wa madeni kutoka kwa wateja wa malipo ya baada ya matumizi, sambamba na ukaguzi wa mita za LUKU kwa wateja wa malipo kabla.
Kampeni hiyo imeanza kutekelezwa katika maeneo yote ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, amesema kampeni hiyo inalenga kuwahimiza wateja waliolimbikiza madeni kulipa kwa hiari kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “Huduma Endelevu Huanzia na Wewe”, ikilenga kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika kulinda miundombinu ya umeme, ambayo ni mhimili muhimu wa maendeleo ya Taifa.
Aidha, Gowelle amesisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu ya umeme si jukumu la TANESCO pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi.
Social Plugin