
Na Deogratius Koyanga, akiripoti kutoka Same, Kilimanjaro
Vumari, SAME — Katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Taarifa na Maarifa (Knowledge Centre - KC) katika Kata ya Vumari, Halmashauri ya Wilaya ya Same, mafanikio makubwa yameanza kuonekana kupitia Mradi wa Women in Rural Cultivating Changes (WRCC). Mradi huu unatekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Shirika la PELUM Tanzania, kwa ufadhili wa Shirika la SeedChange.
WRCC umeleta mabadiliko ya msingi katika maisha ya wanawake na jamii kwa ujumla, hasa katika maeneo ya vijijini ambayo ardhi yake imepoteza uasilia wake kutokana na matumizi yasiyo endelevu na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo maeneo ya nusu jangwa kama Same.
Kwa mujibu wa Felista Msemo, Mwenyekiti wa KC Vumari: “Tulipoanza kazi ya uraghibishi mwaka 2022, tulihamasisha wanawake kupitia vikundi vya VICOba, vya wakulima, na pia kushiriki kwenye mikutano ya vijiji na vyama vya siasa. Matokeo yake, kwenye Halmashauri ya Kijiji cha Vumari pekee, kati ya wajumbe 25, wajumbe 13 ni wanawake, na watatu kati yao ni wana KC.”
Mbali na ushiriki wa wanawake kwenye uongozi, wanawake wamekuwa mstari wa mbele kudai uwajibikaji kutoka kwa viongozi. Naelijwa Msemi, mwana KC kutoka Vumari, anasema:
“Sasa wanawake tunakwenda kwenye vikao kwa wingi, tunahoji kuhusu mapato na matumizi ya kijiji, tunatambulika kama wanawake jasiri na wabunifu wa maendeleo.”
Bi. Nakundwa Emmanuel, mwanachama wa KC na mkulima kutoka Vumari, anaeleza mafanikio yake kupitia Kilimo Ikolojia:
“Kabla ya kujiunga na KC, nilikuwa navuna magunia matatu tu ya mahindi kwa nusu heka. Sasa, navuna hadi magunia sita hadi saba, natumia fedha kujenga nyumba na kumsomesha mwanangu chuo kikuu NIT. Pia tunapata lishe bora kwa kilimo cha mbogamboga.”
Mradi wa WRCC umehamasisha matumizi ya mbegu asilia, kilimo kisichotegemea kemikali, na mbinu za uhifadhi wa rutuba ya ardhi – mambo ambayo yanasaidia kuirejesha ardhi katika uasilia wake na kupambana na athari za tabianchi. Wanawake wanashiriki katika uanzishaji wa benki ya mbegu, mashamba darasa ya ikolojia, na kujifunza kupitia maonyesho ya kijamii.
“Badala ya kutumia pesa kununua mbegu na viuatilifu, sasa fedha hizo zinatumika kwa mahitaji ya familia. Tumepunguza umasikini na kupambana na GBV,” anasema Felista Msemo.
Kwa mujibu wa KC, matukio ya ukatili wa kijinsia sasa yanaripotiwa kwa wingi. Lakini hii si kwa sababu yameongezeka, bali kwa sababu jamii sasa ina uelewa na ujasiri wa kutoa taarifa.
“Watoto wa shule za msingi sasa wanajua KC ni Dawati la Jinsia. Wanaripoti matukio ya ukatili, hata wa kingono,” anasema Felista.
Mfano wa mafanikio hayo ni kesi ya kubakwa kwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza. Kwa ushirikiano wa KC, serikali ya kijiji, afisa ustawi wa jamii, na polisi, mtuhumiwa alikamatwa na kufungwa miaka 30 jela.
KC pia imeshirikiana na wazee wa mila na mangariba kufundisha njia mbadala za kuendesha unyago bila ukeketaji.
“Tunatumia ngoma ya jadi ya ‘Mbere’ kuhamasisha jamii kuhusu maadili, na sio tena kwa kuendeleza mila ya ukeketaji,” alisema mwanachama mmoja wa KC.
Kupitia mabunge ya jamii na semina za jinsia (GDSS), wanawake wamepatiwa elimu kuhusu haki ya kumiliki ardhi. Mradi wa upimaji ardhi katika vijiji vya Vumari na Kizungu umewezesha wanawake wengi kupewa hati miliki.
“Sisi wanawake tulikuwa hatumiliki ardhi. Baada ya elimu, wanaume wameelimika. Sasa tunamiliki ardhi, tumeshalipia hatimiliki zetu,” anasema Sophia Daniel, mwana KC kutoka Vumari.
Hatua hizi zinaendana na utekelezaji wa sera na sheria za kitaifa kama Sera ya Taifa ya Ardhi ya 1995, Sera ya Jinsia ya 2000, na Sheria ya Ardhi Na. 4 ya 1999 inayotambua usawa wa wanawake na wanaume katika umiliki wa ardhi.
Pia inatekeleza malengo ya Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo (FYDP III) ambao unasisitiza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi na ulinzi wa mazingira.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Vumari, Kenedy Mahega, anasema:
“Tangu nianze kazi hapa mwaka 2018, sijawahi kuona mwamko mkubwa wa wanawake kama sasa. KC hii ya Vumari ni kama jeshi la maendeleo. Wanashirikiana nasi hadi ngazi ya vitongoji, wanafanya kazi ambazo awali zingefanywa na serikali pekee.”
KC hushirikiana na serikali za vijiji kuelimisha jamii, kutembelea shule, kuendesha mafunzo, na hata kuchangia uboreshaji wa huduma za afya. Mfano mzuri ni kijiji cha Kizungu, ambapo KC imehamasisha uboreshaji wa chumba cha mama na mtoto katika zahanati ya kijiji hicho.
Pia wanawake sasa wanauwezo wa kugharamia usafiri (bodaboda) kushiriki vikao vya maendeleo, kutokana na kipato kinachotokana na mazao ya kilimo hai.
Mradi wa WRCC umethibitisha kwamba uwekezaji wa kweli kwa wanawake wa vijijini huzaa matokeo makubwa. Kupitia uraghibishi wa kijinsia na ujenzi wa maarifa ya ikolojia, jamii zinazokaa maeneo yenye changamoto za kimazingira na kiuchumi kama Same, zimeanza kufufua ardhi yao, kurejesha uzalishaji, na kupunguza utegemezi wa misaada.
Kwa mujibu wa Mradi wa WRCC, jitihada hizi zinaunga mkono utekelezaji wa Ajenda ya Kitaifa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia, na malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) kuhusu hatua za jamii za kienyeji katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Social Plugin