
Baadhi ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UVCCM) wakifanya usafi katika Kituo cha Afya Sina Kata ya Mafisa Mkoani Morogoro
Na mwandishi wetu Malunde 1 blog -Morogoro
Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Mafisa, mkoani Morogoro, imefanya zoezi la usafi katika Kituo cha Afya Sina kwa lengo la kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi.
Zoezi hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Diwani wa Kata ya Mafisa, Mhe. Joeli Kisomi, Katibu wa CCM wa Kata Bi. Mary Maunganya, na Katibu wa Wazazi wa Kata hiyo, Ndugu Hamisi Kitura.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo, Katibu wa UVCCM Kata ya Mafisa, Yungura Chubwa, amesema lengo kuu la kufanya usafi ni kupunguza nyasi na uchafu unaozunguka kituo cha afya ili kuboresha hali ya mazingira na kuwawezesha wagonjwa kupata huduma katika mazingira safi na salama.
Ameeleza kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kuleta maendeleo kupitia ushiriki wao kwenye shughuli za kijamii.
Chubwa amesisitiza kuwa zoezi hilo halitakuwa la mwisho, kwani UVCCM wamejipanga kuendelea na kampeni ya usafi katika maeneo mengine yenye changamoto ya mazingira.
Ameongeza kuwa wanatambua mchango wao kama vijana katika kujenga jamii iliyo safi na yenye afya bora, na hivyo wataendelea kujitolea katika shughuli kama hizo mara kwa mara.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Kata ya Mafisa, Bi. Mary Maunganya, ameipongeza jumuiya ya vijana kwa hamasa waliyotoa kwa wenzao kushiriki katika zoezi hilo la kijamii.
Amesema kuwa ushiriki wa vijana katika shughuli kama hizo unaonyesha uzalendo na uelewa mkubwa juu ya mchango wao katika maendeleo ya kata.
Aidha, Bi. Maunganya amemshukuru Diwani wa Kata ya Mafisa Mhe. Joeli Kisomi, kwa kuendelea kuwaunga mkono vijana na kutoa mchango wake kwa shughuli hiyo, hali iliyowapa ari vijana hao kufanya kazi kwa bidii na mafanikio.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi na vijana ni chachu ya maendeleo ya kweli katika jamii.

Social Plugin