
Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Charles Hilary, amefariki dunia alfajiri ya leo Mei 11, 2025.
Charles pia aliwahi kuwa mtumishi mwandamizi wa Azam Media Limited kati ya mwaka 2015 na 2023. Alihitimisha muda wake akiwa Mkuu wa Idara ya redio ya UFM, baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameandika:
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Bw. Charles Hilary, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu Zanzibar kilichotokea leo Mei 11, 2025.
Ninatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, familia, ndugu, jamaa na marafiki na wadau wote wa sekta ya habari nchini kwa msiba huu.
Ndugu Charles Hilary atakumbukwa kwa mchango wake adhimu wa zaidi ya miaka 40 katika kukuza sekta ya habari nchini tangu akiwa redioni hadi kwenye televisheni, pamoja na unasihi kwa wanahabari wachanga.
Namuomba Mwenyezi Mungu aijaalie familia yake uvumilivu na subra katika kipindi hiki kigumu, na ailaze roho ya mpendwa wetu mahala pema.
Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea."
Social Plugin