
Na Regina Ndumbaro-Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa jitihada kubwa walizofanya katika ujenzi wa soko la madini lililopo Tunduru, mkoani Ruvuma.
Akizungumza leo katika Baraza la Bunge jijini Dodoma baada ya kupata nafasi ya kuzungumza na Naibu Spika, Mpakate amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kulizindua soko hilo lililojengwa kupitia ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP).
Pia amempongeza Waziri wa Madini kwa kusimamia ipasavyo kufunguliwa kwa soko hilo pamoja na Mkurugenzi na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa kuridhia ujenzi wa soko hilo.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa soko hilo, Mpakate amesema halmashauri ilikuwa na kiwanja tu, lakini wadau walijitokeza na kutumia fedha zao kujenga soko kwa kutumia mkandarasi waliomchagua wao wenyewe.
Amemtaja kijana aliyejenga soko hilo kuwa ni mkazi wa Tunduru aitwaye Abdukaridi, na kueleza kuwa soko hilo limejengwa kwa ubora wa hali ya juu na sasa linahudumia wanunuzi wengi kutoka maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mpakate, asilimia 99 ya eneo la soko hilo tayari limechukuliwa na wanunuzi, na kulifananisha na "Zurich" ya ukanda wa kusini kutokana na umuhimu wake mkubwa kiuchumi.
Hata hivyo, Mbunge huyo ametaja changamoto zinazolikabili soko hilo, ikiwemo baadhi ya wanunuzi kugeuza eneo hilo kuwa ofisi na kufanya biashara ya madini katika nyumba zao binafsi.
Amesema hali hiyo inachangiwa na wachimbaji wadogo kutokuwa na mitaji, hivyo kulazimika kuuza madini kwa madalali wanaowakopesha, jambo linalozorotesha malengo ya msingi ya kuwa na soko la madini.
Licha ya changamoto hizo, ameipongeza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kwa juhudi zao za kudhibiti hali hiyo, ingawa wamekuwa wakizidiwa nguvu.
Katika hatua nyingine, Mpakate amemuomba Naibu Spika wa Bunge kusaidia kupatikana kwa mitambo ya kuchimba madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo, hasa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambako madini aina ya gemstone na kopa yanapatikana kwa wingi.
Amesema mitambo hiyo itasaidia sana kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo katika kutambua maeneo yenye madini kwa urahisi zaidi na kuongeza tija kwenye shughuli zao.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuwapatia mikopo ili waondokane na utegemezi kwa madalali.
Social Plugin