Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKAGUZI WA USHIRIKA MKOA WA RUVUMA ATOA MAFUNZO YA USIMAMIZI NA UHASIBU KWA VYAMA VYA USHIRIKA MBINGA NA NYASA


Mkaguzi wa Ushirika Jackson Sinde akitoa Mafunzo ya Usimamizi na Uhasibu kwa Vyama vya Ushirika Mbinga na Nyasa katika ukumbi wa Mbicu Hotel Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma
Wajumbe wakiwa kwenye mafunzo
Wajumbe wakiwa kwenye mafunzo

Na Regina Ndumbaro Mbinga-Ruvuma 

Katika juhudi za kuimarisha usimamizi wa fedha na uwajibikaji ndani ya vyama vya ushirika, Mkaguzi wa Ushirika Mkoa wa Ruvuma, Bw. Jackson Sinde kutoka Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Ruvuma(COASCO)ameendesha mafunzo kwa watendaji na wajumbe wa bodi wa vyama vya ushirika katika halmashauri za Mbinga Mji, Mbinga Vijijini na Nyasa. 

Mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu juu ya taratibu za uhasibu, umuhimu wa ukaguzi wa hesabu, na wajibu wa bodi katika kulinda mali za vyama kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya ushirika.

 Mafunzo hayo yamefanyika kwa watendaji wa vyama ambapo wamekumbushwa umuhimu wa kuzingatia taratibu za uhasibu kwa uwazi na usawa katika miamala ya kifedha. 

Vilevile, wameelekezwa namna bora ya kujiandaa kwa ajili ya ukaguzi wa hesabu unaofanywa na COASCO na kuhamasishwa kujiendeleza kitaaluma ili kuongeza uwezo wao wa kutekeleza majukumu ya kila siku kwa ufanisi.

Tarehe 07 Mei 2025, mafunzo hayo yameendelea katika ukumbi wa Mbicu Hotel ambapo yamewahusisha wajumbe wa bodi waliopata mwongozo wa kusimamia kwa karibu utendaji wa watendaji, kuhakikisha taarifa za kifedha zinaandaliwa kwa wakati na kwa usahihi, na kuhakikisha zoezi la ukaguzi linafanyika kwa mujibu wa ratiba. 

Pia wamesisitizwa kuwajibika kwa kuhakikisha vyama vyao vinafuata miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa ushirika.

Hata hivyo, changamoto kubwa iliyobainika ni kuwepo kwa vyama takribani 30 kutoka halmashauri hizo tatu ambavyo bado havijawasilisha taarifa za fedha na nyaraka muhimu kwa ajili ya ukaguzi wa hesabu, licha ya kutakiwa kufanya hivyo hadi kufikia tarehe 30 Septemba 2024. 

Hili imeonyesha hitaji la kuimarisha uwajibikaji zaidi na kufuatilia utekelezaji wa wajibu wa vyama hivyo kwa karibu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com