Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIJA FELICIAN: SAFARI YA MAISHA KUTOKA SHIMO LA DHAHABU HADI KILELE CHA HABARI


Shija Felician

Imeandaliwa na Malunde Media

Katika muktadha wa maisha ya dhiki na changamoto za kila siku, jina la Shija Felician linang'ara kama nyota ya matumaini kwa wale wote wanaotafuta njia ya kutoka chini hadi juu.

Ni simulizi ya kweli ya kijana aliyeanzia kwenye migodi, stendi, cherehani, hadi kuwa Mwandishi Nguli / Mwandamizi maarufu na mmiliki wa televisheni ya mtandaoni – Kahama Online TV.

Mwanzo wa Safari: Maisha ya Mitaani na Bulyanhulu

Mwaka 1980, akiwa bado mwanafunzi wa darasa la sita, Shija alilazimika kusitisha masomo na kuanza kutafuta maisha. Alienda kuajiriwa katika Mamlaka ya Pamba Tanzania, ambako alihusika na kazi ya kuchimba visiki katika eneo la Nyang’hwale, walikokuwa wakianzisha kilimo cha pamba akapata shilingi 600 ,akarudi shule mwaka 1981 kuendelea na masomo. 

Alivyomaliza shule ya msingi alifanya kazi ya ndani kama house boy. Wakati huo huo, licha ya hali ngumu ya maisha, aliendelea kujitahidi kwa kuuza kuni mitaani kwa kuwabebea watu kichwani ili kupata kipato cha kujikimu.

Mwaka 1982, akiendelea kuwa house boy akiwa kijana mdogo mwenye ndoto kubwa, Shija alijitosa kwenye uchimbaji wa dhahabu katika mgodi wa Bulyanhulu.

Alizama hadi mwisho wa mashimo kuvunja miamba ya mawe kwa mikono yake mwenyewe, akitafuta mafanikio.

Licha ya dhahabu kuwa nyingi, hakuambulia chochote. Lakini hakuwahi kukata tamaa.

Kuanzia mwaka 1983 hadi 1985, aliingia kwenye biashara ya sigara za magendo stendi.

Maisha haya yaliambatana na visa vya ugomvi – ikiwemo kumpiga mtu aliyekuwa akijiona bingwa wa karate.

Alifikishwa mahakamani, akahukumiwa kifungo cha miezi sita au kulipa faini ya shilingi 1,000.

Alilipa faini, akaachana na maisha ya kihuni na kujikita katika kazi mpya – fundi cherehani.

Mwaka 1986, alijifunza kushona nguo na kujitegemea kwa kipato cha ushonaji.

Lakini hakuwa mtu wa kukaa sehemu moja – akaingia kwenye biashara ya ngozi za magendo hadi Kenya. Mwaka 1989, walikamatwa na magari matatu ya Isuzu yakataifishwa.

Tukio hili likawa sababu ya kuhama kutoka Nyang’hwale hadi Kahama.

Kahama: Cherehani, Karanga na Hadithi

Mwaka 1990, akiwa Kahama, aliendeleza kazi ya ushonaji huku akiendesha biashara ya karanga, akizipeleka hadi Dar es Salaam.

Huko ndiko alikutana na watu waliomfungulia njia ya dunia ya uandishi – akina Kajubi Mkajanga, Kassim Musa Kassim (Wasaa), Sabi Masanja (Bongo), mzee Zaidi Bawiji (Sani), marehemu Niko Yembayo, na Finas Geranija.

Hawa walikuwa vinara wa majarida na vitabu, wakampa moyo wa kuandika.

Mwaka 1992, alianza pia kuvua samaki Sengerema. Lakini bahati haikuwa yake – shehena ya dagaa ilizama ziwani.

Alirudi Kahama kwa kuuza magunia matupu na kuendelea kushona.

Kuibuka Kwa Kipaji: Uandishi wa Habari na Vitabu

Mwaka 1995, alianza kuandika simulizi katika gazeti la Msanii Afrika, kwa msaada wa akina James Nhende, Jack Tana, na Maximilian Ngesi.

Walimtambua kwa uwezo wake wa kipekee wa kuandika vitabu, wakaanza pia kumfundisha uandishi wa habari.

Mwaka 1997, Redio Free Afrika ilipotangaza nafasi za uwakilishi mikoani, Shija aliomba akipeleka vitabu vyake kama vielelezo.

Bila hata kufanyiwa usaili, alichukuliwa moja kwa moja.

Huo ukawa mwanzo wa safari yake kwenye uandishi wa habari.

Kwa kipindi hicho, redio hiyo ina makao Mwanza.

Mwaka 1999, ilipofika Shinyanga, umaarufu wa Shija ulizidi kuenea.

Alijulikana kwa kazi zake za kipekee na mtazamo wa kiuchambuzi.

Uanzishwaji wa SPC (Shinyanga Press Club)

Mwaka 2001, akiwa Kahama, walihamasika kwenda Mgodi wa Bulyanhulu kuomba msaada kwa waandishi.

Wakakumbushwa kuwa msaada hautolewi bila kuwa na umoja rasmi. Ndipo walipoamua kuunda chama – SPC (Shinyanga Press Club).

Walianza na waandishi 12 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa, wakishirikiana na akina Paulo Mabuga na Binamungu.

SPC ilisajiliwa rasmi mwaka 2003.

Mabuga alichaguliwa mwenyekiti lakini baadaye Suleimani Abeid aliyekuwa makamu wake akachukua nafasi, kisha Shija Felician aliyekuwa makamu wa Abeid, akachukua uongozi rasmi mwaka 2003, na kuongoza hadi mwaka 2015, alipoamua kumuachia Kadama Malunde, mmiliki wa Malunde 1 blog, ambaye aliongoza SPC hadi mwaka 2020.

Mwandishi na Mtunzi Maarufu

Shija Felician ameandika vitabu vingi vilivyojipatia umaarufu kupitia gazeti la Heko, kikiwemo:

📍Dhahabu za Bandia

📍Sipendi Tena Karikiti

📍Dhambi ya Anasa

📍Tapeli la Kike / la Kiume

📍Penzi au Kisasi

📍Sikutaki Nimeokoka

📍Operesheni Komesha

📍Msako wa Wauaji

📍Paja la Shemeji

Vitabu vya watoto:

📚Mjusi Kafiri na Muwindaji

📚Ndege Aliyeoa Binadamu

📚Kisa cha Ngedere Mjinga

📚Chura Aliyemeza Binadamu

Mhasibu aliyekuwa akimlipa kwa kazi hizo alikuwa marehemu Vedasto Msungu.

 Safari Ya Mshindi

Leo hii, Shija Felician ni mmiliki wa Kahama Online TV, Afisa Habari wa kampuni kubwa, na msimulizi wa maisha ya kweli kupitia kazi zake za kiandishi.

Mambo ni kupambana tu, hakuna kukata tamaa,” anasema Shija. “Nilichimba dhahabu, nikauza sigara, nikashona, nikavua dagaa, nikauza karanga – yote haya yamechangia kuwa nilivyo leo. Vijana wasikate tamaa.”

Simulizi ya Shija Felician ni msukumo mkubwa kwa kizazi cha sasa – kuwa mafanikio yanapatikana kwa juhudi, maono, na kuamini katika uwezo wako.

Kutoka kwenye mashimo ya dhahabu hadi vyumba vya habari, Shija amethibitisha kuwa hakuna kisichowezekana kwa anayejitoa kweli.

#ShujaaWaMaisha #MwandishiWaKweli #KahamaOnlineTV


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com