
Na Masanja Mabula, PEMBA
SIKU ya Uhuru wa Habari Duniani ni siku inayotambuliwa ulimwenguni kote kwa sababu ya umuhimu wake. Kwa kuwa uhuru wa Habari ni haki ya msingi kwa binadamu wote na ndioyo maana Umoja wa Mataifa ukaitangaza Mei 3 ya kila mwaka kuwa ni siku ya Uhuru wa Habari.
Kwa watetezi wa haki za binadamu. Wanahabari na wadau wa habari huiadhimisha siku hii katika mwezi mzima wa Mei kwa kutafakari, kujadili na kutathmini uhuru wa habari ulivyo katika eneo husika.
Kama ilivyo kwa mataifa mengine waandishi wa habari Tanzania Zanzibar huadhimisha siku hiyo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutathmini na kuchochea uwapo wa uhuru wa habari nchini.
Makala hii iliyoandaliwa na waandishi wa habari Kisiwani Pemba imebeba dhima ya kufanya uchechemuzi ilikupata Sheria Mpya ya Habari ya Zanzibar ili uhuru wa habari ulindwe na utekelezwe kama unavyoainishwa katika mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda.
Akizungumza na Makala hii, Rehema Ramadhan Said amesema umefika wakati kwa waandishi wa habari na wadau wengine wa habari kuwa na sheria rafiki ambazo zitakuwa ni msaada kwao wakati wanapotekeleza majukumu yao.
“Tupo katika ulimwengu wenye mabadiliko makubwa kihabari, hivyo tunapaswa kuwa na sheria mpya ambayo itaendana na mazingira ya ukuaji wa teknolijia ya Habari,” anasema.
Naye Khadija Rashid Nassor akizungumzia suala la kukosekana sheria rafiki kwa waandishi wa habari ameshauri mamlaka husika kuharakisha kuupeleka mswada wa sheria mpya ya habari ili ujadiliwe na kuwawezesha kupata uhuru wa kutumia taaluma yao kuihabarisha jamii.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba PPC Bakar Mussa Juma amesema itasaidia waandishi wa habari kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.
“Hofu ya kuweza kufungiwa chombo cha habari au kukamatwa mwandishi wa habari ni moja ya sababu zinazowafanya waandishi wa habari kufanya kazi kwa woga, lakini iwapo sheria hii mpya itapishwa itakuwa mwarubaini wa haya yote,” anasema.
Wadau wa habari nao wamekuwa wakiipigia chapuo sheria mpya na rafiki ya habari ipitishwe wakiamini kwamba itawawezesha kupata taarifa zilizochakatwa kwa ufanisi na zilizojaa maudhui tarajiwa.
Mmoja wa wadau wa habari aliyezungumza na Makala hii ni Omar Mjaka Ali ambaye amesema kukoseka sheria rafiki kwa waandishi wa habari kumewafanya wakose taarifa za uchunguzi kutoka kwa waandishi wa habari.
“Mimi ni mdau mkubwa na mfuatiliaji wa taarifa za habari, kwa kweli imefika wakati nakosa kupata taarifa za uchunguzi zenye kuweza kuleta mabadiliko chanya, kwa sasa kila ukisoma taarifa ni za matukio tu,” anasema.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amesikika akisema kuna mpango wa kuifanyia marekebisho sheria ya habari, lakini ni kama vile kauli hizo zimekuwa za kisiasa.
“Tunategemea sana katika kikao cha bajeti cha Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais tunatarajia kuisoma na kuipitisha sheria ya habari ili nasi Zanzibar tuwe na sheria mpya na rafiki kwa waandishi wa Habari.” Hiyo ndiyo ahadi aliyoitoa Waziri Tabia mwanzoni mwa Aprili mwaka huu wajkati wa Kikao Kazicha Maafisa Habari wa Serikali kilichofanyika Amani Complex mjini Unguja.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamesema kuwepo kwa sheria mpya na rafiki ya habari haitaleta faida kwa waaandishi wa habari bali itakuwa ni ukombozi wa wadau wote wa masuala ya habari.
Mariam Saleh Juma kutoka Chama Cha Umma, amekizungumza na Makala hii amesema kuwapo kwa sheria mpya itasaidia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa weledi na bila woga.
“Waandishi wa habari kwa sasa najua kwamba mnashindwa kuwa huru kuandika na kutangaza baadhi ya matukio ya kisiasa kutoka vyama vyote vya siasa, hivyo tunashauri sheria ipitishwe ili kukuza demokrasia nchini,” anasema.
Naye Katibu wa Idara ya itikadi na Uenezi wa CCM Jimbo la Micheweni Salim Jabu anasema zipo sheria ambazo ni kikwazo kwa waandishi wa habari, ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho ili ziendane na wakati wa sasa.
Katibu wa ACT Mkoa wa Chake Chake Saleh Nassor Juma, ameshauri mamlaka husika kuharakisha kuipitisha sheria mpya ya habari ili kuwafanya waandishi na wadau wengine wa habari kuwa huru kutekeleza majukumu yao.
Amefahamisha mwarubaini wa changamoto zinazokwamisha uhuru wa habari na zinaweza kumalizwa na uwepo wa sheria mpya ambayo itakuwa rafiki na yenye kuleta tija kwa waandishi na wadau wa habari,
“Nina imani waandishi wa habari muda sio mrefu mtapata sheria mpya ambayo itakuwa rafiki katika utendaji kazi wenu, hivi juzi nilimsikia waziri mwenye dhamana ya habari akitoa tamko la kupitishwa sheria mpya kwenye mkutano wa maafisa habari wa serikali,” anafahamisha.
Si waandishi wa habari pekee wanaohitaji kuwapo kwa sheria mpya na rafiki ya habari visiwani Zanzibar bali hata wadau wa habari wakiwamo wana harakati na watetezi wa haki za binadamu n ahata wananchi kwa sababu kupata Habari na kutoa maoni yao ni miongoni mwa haki zao za msingi.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem, amesema katika kikao cha 10 cha Baraza la Wawakilishi , mkutano wa 19, Baraza litajadiliwa miswada miwili ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 – 2026 na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya mwaka 2025-2026.
Taarifa hiyo inazima ndoto za waandishi wa habari na wadau wa habari visiwani Zanzibar ya kupata Sheria Mpya ya Habari ambayo ni rafiki na itakayo wawezesha kufanya kazi zao kwa uhuru na weledi.
Social Plugin