Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. TULIA APONGEZA MAFUNZO YA SAMIA LEGAL AID JIJINI MBEYA

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akizungumza jambo na Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mhe. Damas Ndumbaro Jijini Mbeya
Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akizungumza na wananchi wa Jiji la Mbeya wakati wa kufunga mafunzo ya elimu ya msaada wa kisheria wa Mama Samia Legal Aid jijini humo
Wananchi waliojitokeza kupata elimu hiyo ya Mafunzo ya Msaada wa Kisheria viwanja vya Shule ya Msingi Asanga Uyole Mkoani Mbeya

Na Regina Ndumbaro, Uyole - Mbeya

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo ya elimu ya msaada wa kisheria kupitia mpango wa Samia Legal Aid, amewapongeza wananchi wa Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku nne mfululizo katika viwanja vya Shule ya Msingi Asanga, Uyole jijini Mbeya.

Dkt. Tulia amesema kuwa elimu hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi, kwani imewasaidia kuelewa haki zao, namna ya kukabiliana na changamoto kama ukatili wa kijinsia, migogoro ya kifamilia, mirathi, pamoja na kuimarisha ushiriki wao katika masuala ya uchaguzi. 

Ameongeza kuwa viongozi wa mitaa, kata na makundi mbalimbali wanapaswa kushirikiana katika kuendeleza elimu hii kwa jamii.

Aidha, Dkt. Tulia amewasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa mpango huu wa Samia Legal Aid ni sehemu ya jitihada za Rais kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria na elimu ya haki zao bila vikwazo. 

Ameomba mafunzo hayo yawe endelevu kwa kuwa wananchi wameyaelewa na kuyapokea kwa moyo wa shukrani.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Damas Ndumbaro, amewapongeza wataalamu waliotoa elimu hiyo kwa umahiri na kujitolea kwao kuhakikisha wananchi wa Mbeya wanapata uelewa sahihi wa masuala ya kisheria.

Mhe. Ndumbaro amesema elimu hiyo imelenga kutatua migogoro ya kijamii, kukuza utawala bora, na kuandaa jamii yenye uelewa wa masuala ya uchaguzi. 

Amewasihi wananchi kuendeleza amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu, huku akiahidi kuwa Wizara yake itaangalia uwezekano wa kuendeleza mafunzo hayo kwa mikoa mingine nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com