Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Hassan Linyama
Wananchi waliojitokeza kupata elimu ya msaada wa kisheria wa mama samia Legal Aid Halmashauri ya Madaba
Mwanasheria Fedrick Makamba akiendelea kutoa elimu ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia Legal Aid Kata ya Gumbiro Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro Madaba-Ruvuma
Katika muendelezo wa kampeni ya kisheria ya Mama Samia Samia Legal Aid, wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba wamenufaika kwa kupatiwa elimu ya msaada wa kisheria.
Kampeni hiyo, chini ya uongozi wa Mbunge wa Jimbo la Madaba, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, imefikisha elimu kwa wananchi wa Kata ya Gumbiro na Kata ya Mkongotema.
Elimu hiyo imetolewa na Sista Winfrida Masiaga na Fedrick Makamba, ambapo wametoa mafundisho juu ya mirathi ikiwa ni pamoja na namna ya kupata haki ya mirathi na masuala muhimu ya kuzingatia.
Vilevile, wananchi wamefundishwa kuhusu utawala bora na umuhimu wa uwajibikaji katika jamii.
Katika kipindi cha maswali na majadiliano, mmoja wa wananchi, Clever Mwandila, ameiomba serikali kuangazia changamoto zinazotokana na uzalishaji usiofuata mpango wa uzazi katika jamii za wafugaji.
Pia ameuliza kuhusu mamlaka ya urithi pale ambapo mmoja wa wanandoa amefariki.
Maswali haya yamejibiwa kikamilifu na jopo la wanasheria waliotoa huduma hiyo ya msaada wa kisheria.
Wananchi wamepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wao Mheshimiwa Mhagama kwa kuwawezesha kupata elimu hii muhimu ambayo imewasaidia kuelewa vizuri masuala ya urithi, ugawaji wa mali, na utawala bora.
Kwa upande wake, Mratibu wa kampeni hiyo, Hassan Linyama, amesema lengo kuu la Samia Legal Aid ni kusaidia jamii zisizo na uwezo wa kugharamia huduma za mawakili ili ziweze kupata haki kwa njia mbadala, ikiwemo kupata uwakilishi wa kisheria bure.
Amebainisha kuwa kampeni hiyo imelenga kufika katika kata zote nane za Halmashauri ya Madaba.
Social Plugin