
Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mhe. Damas Ndumbaro akigawa vifaa vya michezo.
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, ametangaza kuanzishwa kwa mashindano ya mpira wa miguu ya Ndumbaro Cup, yatakayofanyika hivi karibuni katika jimbo hilo.
Tangazo hilo amelitoa leo Mei 12, 2025, wakati wa hafla ya kugawa vifaa vya michezo kwa matawi ya CCM, ikiwa ni pamoja na mipira 96 na seti za jezi 96.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Ndumbaro amesema kuwa mashindano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambayo inaelekeza vijana kushiriki kikamilifu katika michezo ili kukuza vipaji na kuimarisha afya.
Amesisitiza kuwa michezo ni njia bora ya kuwaweka vijana mbali na vishawishi, na kuwapa fursa ya kujifunza nidhamu, mshikamano na kujituma.
Waziri Ndumbaro ameeleza kuwa mbali na kujenga afya na mshikamano, Ndumbaro Cup itatoa fursa kwa vijana kuonekana na kuvumbuliwa na timu kubwa zinazoshiriki ligi mbalimbali kitaifa.
Hii ni hatua muhimu ya kukuza uchumi wa vijana kupitia michezo, kwa kuwa wale watakaofanya vizuri wataunganishwa na timu za juu, hivyo kupata nafasi ya kujiendeleza zaidi.
Mashindano haya yanatarajiwa kuleta hamasa kubwa kwa vijana wa Songea Mjini, huku pia yakiwa chachu ya amani na utulivu katika jamii.
Kupitia Ndumbaro Cup, jimbo linatarajia kuona mabadiliko chanya katika maendeleo ya michezo na maisha ya vijana kwa ujumla.

Social Plugin