Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATA YA SOMANGA YATEKELEZA MAFANIKIO YA USAJILI WA KADI ZA CCM KIELEKTRONIKI

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM Kata ya Somanga Wilayani Kilwa Mkoani Lindi wakichukua kadi zao za kielektroniki

Na Regina Ndumbaro Kilwa-Lindi 

Katika kuendeleza juhudi za kidigitali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Somanga imeanza rasmi ugawaji wa kadi za uanachama kwa mfumo wa kielektroniki. 

Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Ndugu Salum Winda, amefanya ziara fupi kutembelea maeneo ya utoaji wa kadi na kueleza kuridhishwa kwake na mwitikio mkubwa wa wanachama waliojitokeza kuchukua kadi hizo. 

Amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa usimamizi wake mahiri uliowezesha utekelezaji wa mfumo huo wa kisasa kufanikiwa.

Winda ameeleza kuwa mfumo huu wa kadi za kielektroniki umerahisisha sana mchakato wa ulipaji wa ada za uanachama, ambapo mwanachama anaweza kufanya malipo kupitia simu ya mkononi au benki bila usumbufu. 

Amesisitiza kuwa mfumo huo unahakikisha uwazi, ufanisi, na usalama wa taarifa za wanachama, na hivyo kuimarisha zaidi uimara wa chama katika ngazi za mashina.

Kwa upande wake, Otin Rajabu Mbonde, mjumbe wa serikali ya kijiji, ameipongeza CCM kwa kuanzisha mfumo huo wa kisasa, akisema kuwa ni hatua ya maendeleo inayomwezesha kila mwanachama kupata huduma kwa ukaribu bila kuhangaika. 

Amesema maeneo ya mashina yanayohusika na utoaji wa kadi yamewekwa karibu na wananchi, jambo lililosaidia kupunguza gharama na muda wa kufuata kadi hizo.

Naye Chande Namba, msimamizi mkuu wa Tarafa ya Miteja kutoka Idara ya TEHAMA, ameeleza kuwa zoezi la ugawaji wa kadi katika mashina ya Kata ya Somanga linaendelea vizuri. 

Amewataka wanachama kufika katika maeneo waliyosajiliwa kuchukua kadi zao, huku akiwataka wanaobaini makosa katika taarifa zao wafike kurekebishiwa, na pia kuwaalika wanachama wapya kujiandikisha ili kujiunga rasmi na chama hicho.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com