
Na Lydia Lugakila -Kyerwa
Wananchi katika Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera ya wilaya ya kyerwa wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogezea karibu huduma ya msaada wa kisheria kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ijulikanayo kama Samia Legal Aid Campaign kwani imemulika migogoro mingi ikiwemo ya ndoa na ya ardhi.
Pongezi hizo zimetolewa na baadhi ya wananchi katika kijiji cha Kibimba kata ya Mabira waliojitokeza katika kampeni hiyo.
Philbat France na Mathayo Bernard wamesema kuwa ujio wa kampeni hiyo katika ngazi ya vijiji inaenda kuwa mkombozi kwani familia nyingi zipo katika hali mbaya juu ya migogoro ikiwemo ya ndoa huku wakimtaja Rais Samia kuwa Mkombozi wao.
Wameongeza kuwa familia nyingi zimekuwa na changamoto ya migogoro ya ndoa inayosababishwa na watoto wao wenyewe ambayo mwisho wa siku inasababisha migogoro ya ardhi mpaka kusababisha kufanyiana vitendo vibaya wakati mwingine, kwani asilimia kubwa ya waathirika katika mgogoro hiyo ni wanaume hasa pale wanapopigwa na wake zao.
Pia wamesema kupitia uelewa walioupata kutoka kwa Wataalam hao itasaidia kukuza malezi bora ya familia zao hasa kwa watoto na kuwa na uelewa juu ya mirathi katika familia zao.
Naye Getruda Mwiga kutoka dawati la jinsia na watoto ambaye naye ni miongoni mwa timu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ambapo amewasihi wazazi kudumisha malezi bora kwa watoto wao kwani hiyo itasaidia kuondoa changamoto hizo katika jamii.
“Malezi bora kwa watoto wetu ni muhimu pia kama familia tunatakiwa kusikiliza na unapopata changamoto usisite kutoa taarifa ili kupata msaada mfano kwa wakina Baba najua mnakutana na changamoto nyingi huko katika makazi yenu ila msiwe na aibu kutoa taarifa kwani itawasaidia kutojichukulia sheria mkononi”,amesema.
Kwa upande wake Afisa ardhi mwandamizi Bw. Bitabonwa Mkama amesema kila mwananchi anayo haki ya kumiliki ardhi kisheria bila kubagua jinsia na kupitia kampeini hiyo ya msaada wa kisheria itakuwa ni fursa kupata msaada zaidi.
Sambamba na hayo pia Bitabonwa katika kutoa elimu hiyo ya msaada wa kisheria juu ya umiliki wa ardhi amekutana na changamoto ya kutokuwepo kwa mabaraza ya ardhi ya vijiji jambo linalopelekea migogoro mingi ya ardhi katika vijiji hivyo ambapo ameahidi jambo hilo kufanyiwa kazi kupitia kampeni hiyo.


Social Plugin