Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AMWAGA BILIONI 45 KUTATUA TATIZO LA MAJI JIJI LA DODOMA



Na Maandishi wetu Dodoma.

Waziri wa Maji Mh. Jumaa Aweso amesema Rais Dkt. Samia Suluh Hassan ameelekeza utekelezaji wa miradi ya maji yenye thamani ya Tsh Bilioni 45 kutatua changamoto ya Maji Jijini Dodoma wakati ikisubiriwa utekelezaji wa Miradi ya kuleta maji kupitia Ziwa Victoria na mradi wa Bwawa la Farkwa.

Waziri Aweso ameyasema hayo wakati akishuhudia utiaji wa saini wa mkataba wa mradi wa kusambaza maji kupitia visima vya maji vya Nzuguni A wenye thamani ya Tsh 5bn unaotarajiwa kuwanufaisha watu 123,095.

“Mbunge wenu alileta maombi kwa Mh. Rais Samia juu ya uchimbwaji wa visima virefu wakati wa mkutano wa Mh. Rais pale Mpunguzi na sisi Wizara tukapata maelekezo ambayo tumeyafanyia kazi.

Tunamshukuru Mh. Rais Samia kwa kulivalia njuga suala la maji hapa Jijini Dodoma kwa kuelekeza utekelezaji wa miradi ya maji ya zaidi Tsh 45bn ambayo itasaidia sana kupunguza tatizo la mgao wa maji katika maeneo mbalimbali.

DUWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine kama vile Nala 3.8bn UDOM,(1.2bn), Mji wa Serikali (35.6bn), n.k. Aidha wizara ya maji kwa kushirikiana na taasisi

zake (DUWASA na RUWASA) imeunda timu zinazo endelea na Utafiti wa Maji chini ya Ardhi na Uchimbaji wa visima katika maeneo ya Mzakwe, Nzuguni, Kisasa, Nkuhungu,Miganga, Zuzu, Msalato na Ihumwa.

"Nipo hapa Jijini Dodoma na kesho naanza ziara maalum kukagua utekelezaji wa miradi hii ili wananchi wa Dodoma wapate maji ya uhakika”amesema Aweso

Kwa upande Wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma ambaye pia ni Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema utekelezaji wa mradi ya usambazaji wa maji utasaidia kupunguza adha ya mgao wa maji kwa wananchi wa maeneo ya nzuguni Nkuhungu,Miganga,Chidachi, Kisasa-Bwawani,Mwangaza, Ipagala, Ilazo, na Swaswa, Mpamaa na Njedengwa.

Awali akitoa taarifa yake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA) Eng. Aron Joseph amesema Mradi huu unalenga kuhudumia wananchi wapatao 123,095 katika maeneo yaliyotajwa

Aidha Eng Aron amesema Kukamilika kwa mradi huu kutapelekea ongezeko la uzalishaji kutoka lita milioni 81 hadi 91 kwa siku sawa na ongezeko la 30% kutoka chanzo cha Nzuguni.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com